1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa EU waionya China kuhusu uhusiano wake na Urusi

30 Machi 2023

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya,Ursula von der Leyen ameionya China kuwa msimamo wake katika vita vya Urusi huko Ukraine ndio utakaomua uhusiano wao.Amesema Ulaya haitazamii kuvunja uhusiano na Beijing.

Ursula von der Leyen / Rede 30.03.2023
Picha: VALERIA MONGELLI/AFP/Getty Images

Wiki ijayo, Von der Leyen ataambatana na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron hadi mjini Beijing wakati viongozi wa Umoja wa Ulaya wakitarajia kufanya mazungumzo na Rais Xi Jinping wa China.

Ziara hiyo, pamoja na nyingine ya Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez inayoanza leo Alhamisi, inajiri baada ya Xi kudhihirisha mshikamano na Rais wa Urusi Vladimir Putin huko Moscow wiki iliyopita.   

China imekuwa ikijinadi kuwa mpatanishi asiyeegemea upande wowote na kwamba imeweka mezani kile inachoeleza kama mpango wa kusaidia kusitisha mapigano. Lakini imekataa kulaani wazi wazi vita vya Moscow na imekuwa ikionywa na nchi za Magharibi dhidi ya hatua zozote za kutuma silaha nchini Urusi.

Soma pia: Putin asema yuko tayari kuujadili mpango wa China kuhusu Ukraine

Wizara ya ulinzi ya China imesema hii leo kuwa Jeshi lake lipo tayari kushirikiana na jeshi la Urusi ili kuimarisha uratibu na mawasiliano ya kimkakati. Tan Kefei, msemaji wa wizara ya ulinzi ya China amesema katika mkutano na waandishi wa habari kuwa nchi hizo mbili zitafanya kazi pamoja na kuendesha luteka ya kijeshi ili kutekeleza na kulinda mipango ya kimataifa ya usalama.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen Picha: John Thys/AFP

Von der Leyen amesema mpango wowote wa amani unaoweza kutekelezeka ni lazima uzingatie masharti ya Ukraine na haupaswi kuisaidia Kremlin kujizatiti katika maeneo iliyo yanyakua kinyume cha sheria.

EU yakinzana na matakwa ya Marekani kuhusu China

Umoja wa Ulaya unajaribu kuwa na msimamo wake kuihusu China wakati Marekani ikiwashinikiza washirika wake wa Ulaya kujiunga na msimamo wake mkali zaidi dhidi ya China. 

Mataifa yenye uwezo mkubwa kiuchumi barani Ulaya kama vile Ufaransa na Ujerumani yameonesha nia ya kutotaka kuvunja uhusiano wa kibiashara na China, wakati nchi za mashariki mwa Ulaya zikiwa na misimamo mikali zaidi.

Wakati hayo yakijiri, Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti Nishati ya Atomiki (IAEA) Rafael Grossiamesema siku ya Jumatano kuwa alikuwa akifanyia kazi mpango wa maelewano juu ya kupatikana usalama katika kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia kinachodhibitiwa na Moscow na kuonya kuhusu kuongezeka kwa shughuli za kijeshi zilizo karibu na eneo hilo.

Mkuu wa IAEA, Rafael GrossiPicha: RIA Novosti/SNA/IMAGO

Grossi ameelezea matumaini kwamba Urusi na Ukraine zitakubaliana juu ya kanuni za usalama karibu na kinu hicho cha Zaporizhzhia, na kuongeza kuwa ziara yake ya kukitembelea kinu hicho ilikuwa ya manufaa makubwa mno.

Soma pia: Xi, Putin wasifu enzi mpya ya mahusiano kati ya mataifa hayo mawili

Aprili mosi, Urusi itachukua urais wa kupokezana katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hatua iliyolaaniwa leo hii na Ukraine ambayo imesema dunia haitokuwa eneo salama ikiwa Urusi itachukua wadhifa huo wa muda.

Nchi wanachama 15 hupokezana Urais huo kila mwezi. Licha ya kwamba Urusi itakuwa na ushawishi mdogo kwenye maamuzi lakini itakuwa na wajibu wa kuamua ajenda zitakazojadiliwa katika Baraza hilo.