Viongozi wa EU wajadili mlipuko wa kisiasa kuhusu wahamiaji
24 Juni 2018Mazungumzo hayo yanayowahusisha viongozi wa mataifa 16 kati ya 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya yameitishwa kujaribu kuondoa tofauti kuhusiana na mgawanyo wa wahamiaji lakini pia kumsaidia kansela wa Ujerumani Angela Merkel anayekabiliwa na shinikizo ndani ya serikali yake kukaza mtazamo wake wa kiliberali kuhusu hifadhi kwa wakimbizi.
Mkutano huo uliitishwa wiki iliopita kusawazisha mambo kabla ya mkutano mkuu wa kilele uliopangiwa siku za Alhamisi na Ijumaa wiki ijayo. Wakati ambapo mataifa manne ya Ulaya Mashariki yanayopinga uhamiaji yakisusia mkutano huo, Merkel na viongozi wengine wamepunguza matumaini ya makubaliano mapana ya Umoja wa Ulaya, wakisema makubaliano madogo madogo ndiyo yanaweza kuwa njia mbadala kwa sasa.
Mataifa 16 yakiongozwa na Ufaransa na Ujerumani yalikuwa yanajadiliana juu ya nani achukuwe jukumu la kushughulikia wahamiaji wanaowasili barani Ulaya -- hususani kwa sasa nchini Italia, Ugiriki na Uhispania - ni kwa muda gani wanapaswa kuwahudumia na ni kiasi gani washirika wao wa Ulaya wanapaswa kuwasaidia.
'Shehena ya nyama za binadamu!'
Uharaka wa kutafuta suluhisho uliainishwa na masaibu ya meli ya Lifeline, ya pili ya uokozi iliyokwama katika bahari ya Mediterania baada ya Italia na nchi jirani ya Malta kukataa kuipa ruhusa ya kutia nanga. Shirika la hisani la Ujerumani linaloendesha meli hiyo iliyobeba Waafrika 239, lilimkosoa waziri wa mambo ya ndani wa serikali mpya ya Italia Matteo Salvini kuhusiana na maandishi yake katika mtandao wa Facebook alimoitaja meli hiyo kama shehena ya "nyama ya binadamu".
"Mpendwa Matteo Salvini, hatuna nyama kwenye mei hii, bali ni binadamu," lilisema shirika hilo katika taarifa. Katika ishara ya mzozo unaozidi ndani ya Umoja wa Ulaya, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema siku ya Jumamosi kuwa mataifa yanayokataa kupokea wakimbizi yanapaswa kupunguziwa faida zake za uanachama wa Umoja wa Ulaya.
Katika ukosoaji ulioelekezwa kwa Poland, Hungary, Slovenia na Jamhuri ya Czech, alisema "mataifa yanayonufaika pakubwa kutokana na mshikamano wa Umoja wa Ulaya" hayawezi kutumia maslahi binafsi ya kitaifa linapokuja suala la wahamiaji". Mataifa hayo manne ya zamani ya kikomunisti yaliyojitowa katika mazungumzo ya Jumapili, kwa muda mrefu yamepinga kuchukuwa wahamiaji.
Dharura ya uhamiaji ya mwaka 2015
Macron aliighadhabisha Italia, ambayo ndiyo kituo kikuu cha kuwasili wahamiaji, kwa kusema kuwa dharura ya uhamiaji, iliofikia kilele mwaka 2015, ilipita na sasa suala hilo ni la kisiasa zaidi. "Dharura ya uhamiaji inaendelea nchini Italia, kwa sehemu kwa sababu Ufaransa inaendelea kuwarejeshea watu mpakani," alisema naibu waziri mkuu wa Italia Luigi Di Maio katika ukarasa wake wa Facebook, akionya kuwa Macron anahatarisha kuigeuza Ufaransa kuwa "adui nambari moja wa Italia" kuhusu suala hilo.
Tangu kuchukuwa madaraka wiki kadhaa zilizopita, serikali mpya ya Italia imekataa kuzipokea meli za kigeni zilizojaa mamia ya wahamiaji. Baada ya kuikatalia meli ya Aquarius ambayo baadae ilitia nanga nchini Uhispania, serikali mjini Roma iliapa kuizuwia meli ya Lifeline. Pia imeapa kutochukuwa tena watafuta hifadhi zaidi, ikiyalaumu mataifa mengine kwa kuiachia mzigo wa kuwahifadhi maelfu ya wahamiaji wanaowasili huko mara kwa mara.
Msimamo wake umeibua mzozo na Ujerumani na pia ndani ya serikali ya muungano ya kansela Merkel, huku wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wakisema mkutano huo mdogo wa kilele utasaidia kumuokoa kansela. Lakini waziri mkuu wa Luxembourg Xavier Bettel alisema mkutano huo haukuwa na lengo la kumuokoa Merkel bali kutafuta suluhisho la mustakabali wa sera ya pamoja ya uhamiaji na ukimbizi barani Ulaya.
Upinzani mkubwa kutoka kwa wafuasi wa siasa kali dhidi ya sera yake ya kiliberali kuhusu wakimbizi ulimuacha Merkel akiwa dhaifu katika uchaguzi wa mwaka uliopita. Bettel alisema Umoja wa Ulaya umepokea pendekezo kutoka kwa Umoja wa Mataifa kusaidia na uhakiki wa watafuta hifadhi nje ya kanda hiyo.
Shinikizo ndani ya serikali ya Merkel
Katika mgogoro wa karibuni, waziri wake mpya wa mambo ya ndani mwenye msimamo mkali Horst Seehofer amempa muda wa hadi mwishoni mwa Juni kutafuta makubaliano ya Ulaya kupunguza idadi ya wahamiaji wapya. Iwapo hilo litashindikana, ameapa kuwaamuru polisi kuwarejesha wahamiaji, hii ikimaanisha wengine huenda wakarejea nchini Italia.
Chini ya kile kinachojulikana na sheria za Dublin za Umoja wa Ulaya, watafuta hifadhi laazima wasajiliwe katika nchi walikofikia kwanza, mara nyingi mataifa haya ni yale yalio kandoni mwa bahari ya Mediterrania kama vile Italia, Ugiriki na Uhispania. Desemba mwaka jana, viongozi wa Umoja wa Ulaya walikuwa wamepanga mwishoni mwa Juni kuwa muda wa mwisho wa kufanyia mabadiliko sheria hizo kwa kuanzisha mfumo wa kudumu wa kugawana wakimbizi katika mataifa yote ya kanda.
Wakati ambapo makubaliano yanaonekana kushindikana, Ujerumani inasema hivi sasa inataka makubaliano ya mataifa mawili, matatu na mataifa mengi. Merkel alimshawishi waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte kuhudhuria mkutano wa Jumapili kwa kumuambia kuwa mahitimisho ya kabla yaliokuwa yameondolewa, walisema maafisa wa Italia.
Mahitimisho hayo yalihusisha miito ya kuharakisha kurejeshwa wahamiaji katika mataifa yaliowasajili, kama vile Italia, na kusababisha hasira mjini Rome. Mkutano huo ulitarajiwa pia kujadili namna y kuimarisha doria katika mipaka ya nje ya kanda hiyo. Makubaliano ya ushirikiano kati ya Uturuki na Libya kwa sasa yamesaidia kupunguza pakubwa uingiaji wa wahamiaji barani Ulaya tangu kilele cha mwaka 2015 ambapo zaidi ya wahamiaji milioni waliingia.
Hofu ya kusambaratika kwa mfumo wa Schengeni
Viongozi hao pia wamejadili mapendekezo ya kuanzisha vituo katika mataifa nje ya Umoja wa Ulaya ili kutenganisha wakimbizi halali wa kivita na wahamiaji wa kiuchumi, ambao wanaweka kurejeshwa nyumbani. Lakini wakati kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa wahamiaji wapya huko mbeleni, wanadiplomasia wanaonya kuwa mkwamo juu ya mabadiliko katika sera ya wakimbizi unaweza kuharibu mafanikio makubwa zaidi ya Umoja wa Ulaya, mfumo wa usafiri huru ndani ya mipaka ya kanda ya hiyo maarufu Schengen.
Mataifa mengine yaliohudhuria mkutano huo wa kilele ni Austria, Ugiriki, Malta, Bulgaria, Ubelgiji, Uholanzi, Croatia, Slovenia, Denmark, Finland, Sweden na Luxembourg.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri: Daniel Gakuba