1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU wajadiliana kuhusu Brexit na mzozo wa Uingereza na Urusi

Grace Kabogo
23 Machi 2018

Viongozi wa Umoja wa Ulaya leo wanatarajiwa kuweka msingi wa awamu ijayo ya mazungumzo ya Uingereza kujiondoa kwenye umoja huo, unaojulikana kama Brexit.

Belgien EU-Gipfel - Juncker und May
Picha: Reuters/F. Lenoir

Viongozi 27 wa nchi za Umoja wa Ulaya ambao wanahudhuria mkutano huo wa kilele unaofanyika Brussels, Ubelgiji, watapitisha mwongozo wa mazungumzo hayo kuhusu mustakabali wa uhusiano kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya na pia watakubaliana kuhusu kipindi cha mpito cha miezi 21.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May amehudhuria mkutano ambao ulijadili mgogoro wa kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani, lakini hatoshiriki katika mkutano pamoja na viongozi wenzake utakaojadili kuhusu Brexit. Wakati wa chakula cha usiku, May aliwasihi viongozi wenzake kutumia muda huu kukabiliana na maswali magumu kuhusu biashara pamoja na mpaka wa Ireland.

Kipindi cha mpito kinakusudiwa kurahisisha mchakato wa Brexit Machi 2019 na kuongeza muda wa uanachama wa Uingereza katika soko la pamoja la Umoja wa Ulaya, lakini bila ya kuwa na haki ya kupiga kura hadi mwishoni mwa 2020.

Ama kwa upande mwingine, viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuwa Urusi inahusika na shambulizi la sumu dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi nchini Uingereza, Sergei Skripal pamoja na binti yake. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo asubuhi, viongozi hao walijadili kuhusu tukio hilo na kuamua kuiunga mkono tathmini ya Uingereza kwamba Urusi inahusika na shambulizi hilo.

Baadhi ya viongozi wa Umoja wa UlayaPicha: picture-alliance/AP Photo/O. Hoslet

Viongozi hao wamelaani vikali shambulizi hilo la sumu na kuwapa pole wote ambao maisha yao yamo hatarini na wameahidi kutoa msaada katika uchunguzi unaoendelea. Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema wamejadiliana kwa kirefu na wamekubaliana kwamba ushahidi wote unaonesha Urusi inahusika katika shambulizi hilo na hakuna maelezo mengine yoyote.

''Nchi zote wanachama zimekubaliana na mtazamo huu na tutaendelea kuiangalia hali inavyoendelea. Uingereza imetoa taarifa zake zote katika Shirika la kimataifa la kuzuia kuenea kwa silaha za kemikali na tutasubiri matokeo ya uchunguzi huo,'' alisema Merkel.

Awali, Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras aliwaambia waandishi habari kwamba Umoja wa Ulaya unahitaji kuelezea mshikamano wake na Uingereza na kuongeza lakini wakati huo huo, wanahitaji kufanya uchunguzi.

Aidha, Umoja wa Ulaya umemuita balozi wake nchini Urusi kurejea Brussels kwa majadiliano zaidi. Baadhi ya nchi za umoja huo zinafikiria kuwafukuza wanadiplomasia wa Urusi. Hata hivyo, Urusi imekanusha kuhusika na shambulizi hilo, hatua iliyoanzisha mzozo mwingine mkubwa katika uhusiano kati ya Urusi na nchi za Magharibi.

Wakati huo huo, viongozi wa Umoja wa Ulaya wamelaani vikali vitendo visivyo halali vinavyofanywa na Uturuki dhidi ya Ugiriki na Cyprus. Kauli hiyo imetolewa jana baada ya Uturuki kuwakamata wanajeshi wawili wa Ugiriki na kuahidi kuizuia serikali ya Cyprus yenye watu wa asili ya Ugiriki ambayo inatambulika kimataifa, kuchimba mafuta na gesi.

Umoja wa Ulaya umeitaka Uturuki kauchana na vitendo hivyo na kuheshimu haki na uhuru wa Cyprus kugundua, kuchimba na kutumia maliasili zake kwa mujibu wa sheria za Umoja wa Ulaya na zile za kimataifa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, DPA
Mhariri: Josephat Charo