Viongozi wa EU wajaribu kupata muafaka wa ufufuaji uchumi
17 Julai 2020Nchi hizo zina mengi ya kupoteza katika mkutano huu wa kwanza wa ana kwa ana ambao haujafanyika katika hali hiyo kwa miezi kadhaa. Kundi hilo la mataifa linakabiliwa na mdororo mkubwa kabisa wa ukuaji wa uchumi tangu umoja huo kuundwa, na mataifa yanahitaji fedha haraka kujitoa kutoka katika mzozo wa kiuchumi uliosababishwa na janga la ugonjwa wa COVID-19..
Wakati viongozi kadhaa wameeleza matumaini yao kupatikana muafaka wakiwa njiani kuelekea katika mkutano huo wa kilele, uwezekano halisi wa kufikiwa makubaliano leo Ijumaa ama kesho Jumamosi yanaonekana yameporomoka kwa Ujerumani.
Leo Ijumaa, akiwa ni siku yake ya kuzaliwa akitimiza miaka 66, kansela Angela Merkel amesikika akiwa hana imani ya kutosha kwamba mkutano huo wa kilele utapata ufumbuzi kuhusu mfuko wa bilioni kadhaa wa ufufuaji wa uchumi wakati huu wa janga la virusi vya corona.
"Niseme tu kwamba tofauti bado ni kubwa sana. Kwa hiyo siwezi kusema iwapo tutapata matokeo mara hii," Merkel aliwaambia waandishi habari mjini Brussels. Unapaswa kukabiliana na hali halisi."
Muda wa ukweli
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alisema "ana matumaini lakini ya tahadhari" kwamba makubaliano yanaweza kufanyika, "ni muda wa ukweli na dhamira kwa Ulaya."
Merkel na Macron wote walifanya mikutano na viongozi mbalimbali katika wiki za hivi karibuni na wamechukua jukumu la mbele katika kutoa rai kwa mawaziri wakuu kufikia maridhiano.
Msingi wa majadiliano hayo ni pendekezo la rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Charles Michel ambalo linalenga kiwango cha euro bilioni 500 za misaada na euro bilioni 250 za mikopo, hoja hiyo ikiwa katika msingi wa pendekezo la hapo kabla na Halmashauri ya Umoja wa Ulaya.
Alipoulizwa iwapo pendekezo hilo linaweza kupita kirahisi, Rais wa Bunge la Ulaya, David Sassoli alisema, "Umoja wa Ulaya si mashine ya benki (ATM), tuna kitu zaidi cha kusema, sio tu kama watu wa Ulaya, lakini pia mataifa wanachama. Tuna kitu zaidi kuliko kujiangalia tu kama wagawa fedha. Tuna jukumu kubwa kuurejesha uchumi katika hali ya kawaida, kuhakikisha hali bora za raia wetu, uhuru wa maoni ya umma, na kufanya kwa mpango ambao utaruhusu Umoja wa Ulaya kulinda maadili yake."
Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Ulaya ameongeza kuwa makubaliano yanawezekana iwapo viongozi wataweza kupata hamasa ya kisiasa kufanya hivyo.