Viongozi wa EU wakutana bila Uingereza
29 Juni 2016Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk amewaambia wanahabari baada ya viongozi wa nchi wanachama 27 kukutana mjini Brussels bila ya waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, wamekubaliana wazi kwamba kuingia katika soko la pamoja kunahitaji kukubaliwa kwa haki nne za uhuru ukiwemo uhuru wa kusafiri watu, biadhaa, huduma na fedha.
Tusk amesema viongozi 27 wa Umoja wa Ulaya wataandaa mkutano wa kilele – bila Uingereza – mjini Bratislava, Slovakia mnamo Septemba 16 ili kujadili mustakabali wao baada ya uamuzi wa Uingereza kuondoka katika umoja huo "Pia tumejadili suala kwamba watu wengi barani Ulaya hawaradishwi na hali ya sasa ya mambo na wanataraji tufanye mageuzi. Wengi wamekumbusha kuwa kwa miongo mingi, Ulaya ilileta matumaini na kuwa tuna jukumu la kuirudisha hali hiyo. Kama ujuavyo, ulikuwa mkutano wa kwanza wa viongozi 27 baada ya Uingereza kujitoa na hivyo ni mapema kufanya maamuzi".
Mkutano huo utakuja siku chache tu wakati chama tawala cha Kihafidhina nchini Uingereza kikimchagua mrithi wa Cameron, ambaye alijiuzulu wiki iliyopita baada ya nchi yake kupiga kura ya asilimia 52 dhidi ya 48 ya kuondoka katika Umoja wa Ulaya. Waziri huyo mkuu wa zamani wa Poland amesisitiza kuwa mazungumzo kuhusu mahusiano ya siku za usoni ya Uingereza na Umoja wa Ulaya hayawezi kuanza hadi pale itakapoidhinisha mchakato unaochukua miaka miwili ambao utawezesha wao kujitenga.
Akizungumza katika mkutano huo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema viongozi wa Umoja wa Ulaya hawataki kuanza kuyashughulikia mabadiliko magumu ya mikataba ya umoja huo wakati wakilenga kujiimarisha. "tulizugnumza mengi kuhusu mada tatu: usalama, usalama wa ndani na nje, ulinzi wa mipaka yetu ya nje kuhusiana na uhamiaji. Tulizungumza kuhusu kazi, ukuaji uchumi na ushindani. Na tuliangazia suala la vijana barani Ulaya"
Merkel amesema kuwa funzo linalotokana na kujitoa Uingereza sio hasa kuhusu muingiliano mkubwa wa watu au kurejesha mamlaka kwa serikali za kitaifa. Amesema kwa mfano kupambana na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, huenda kukahusisha kufuta maagizo ya Umoja wa Ulaya na kuimarisha ushirikiano wa Ulaya.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Nicola Sturgeon amekutana leo na Rais wa Bunge la Ulaya Martin Schulz na atakutana baadaye na ofisi kuu ya Umoja wa Ulaya, Rais Jean Claude Juncker. Wapiga kura wa Scotland walipiga kwa wingi kura ya kutaka kubakia katika Umoja wa UIaya lakini wakazidiwa nguvu na kura za England. Sturgeon amedokeza kuwa huenda kukawa na kura ya maoni kuhusu uhuru wa Scotland
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu