Viongozi wa EU wakutana Budapest kwa mkutano usio rasmi
8 Novemba 2024Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Budapest nchini Hungary leo katika mkutano wa kilele usio rasmi kutafuta njia za kufufua upya ushindani wa Umoja huo dhidi ya Marekani na China.
Kulingana na rasimu ya taarifa iliyoonekana na shirika la habari la dpa, viongozi hao wa Umoja wa Ulayawanapaswa kuahidi kuchunguza na kutumia mbinu zote kufikia malengo yao. Hata hivyo, wanadiplomasia wa Umoja huo wanasema lugha hiyo haieleweki kimakusudi.
Mkutano huo unafanyika katika uwanja wa mpira wa Puskás huku ripoti kutoka kwa waziri mkuu wa zamani wa Italia Mario Draghi, ambaye pia anatarajiwa kuhudhuria, ikiweka msingi wa mazungumzo hayo.
Pia katika ajenda ya mkutano huo ni uchaguzi wa hivi karibuni huko Georgia na uamuzi wa bunge la Israel kulipiga marufuku Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya kiutu kwa Wakimbizi wa Kipalestina katika Mashariki ya Kati (UNRWA) huko Gaza.