1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa EU wamaliza mvutano kuhusu bajeti

11 Desemba 2020

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamefikia makubaliano kuhusu bajeti ya muda mrefu na mpango wa uokozi wa uchumi baada ya wiki kadhaa za upinzani kutoka mataifa mawili wanachama ya Poland na Hungary

Belgien I EU-Gipfel in Brüssel
Sehemu ya viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels Picha: Olivier Matthys/Pool/REUTERS

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mkutano wa kilele wa viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya unaoendelea mjini Brussels.

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya Charles Michel amesifu hatua iliyofikiwana kusema inatoa nafasi ya kuanza utekelezaji wa bajeti ya kanda hiyo pamoja na kuimarisha tena chumi za mataifa wanachama chini ya mpango wa uokozi unaolenga kufufua shughuli za uzalishaji baada ya janga la virusi vya corona.

Hungary na Poland zilitumia kura ya turufu kuzuia kupitishwa kwa bajeti ya dola Trilioni 1.3na mpango wa uokozi wa dola bilioni 900 kufuatia masharti kuwa utolewaji wa fedha hizo ungezingatia jinsi nchi wanachama zinavyozingatia misingi ya utawala sheria na demokrasia.

Masharti hayo yangeruhusu kuzuiwa nchi mwanachama kupatiwa fedha pindi misingi kadhaa ya demokrasia na utawala wa sheria itakiukwa ikiwemo uhuru wa mahakama au kukosekana uadilifu katika usimamizi wa bajeti.

Poland na Hungary vinara wa kupuuza misingi ya demokrasia 

Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki (kushoto) na mwenzake wa Hungary Viktor Orban wakiwasili kwenye mkutano mjini Brussels Picha: Francois Lenoir/Pool/File Photo/Reuters

Kwa muda mrefu sasa serikali zote mbili za Poland na Hungary zimekalia kuti kavukutokana na wasiwasi unaongezeka kwamba zinatumbukia kwenye utawala kiimla na zinaongoza kupuuza misingi ya kidemokrasia.

Wakosoaji wa makubaliano yaloyopatikana wanaamini Umoja wa Ulaya umetoa nafasi kwa Poland na Hungary kupuuza zaidi utawala wa sheria.

Viongozi wa mataifa hayo mawili kwa pamoja wameyakaribisha kwa bashasha makubaliano yaliyofikiwa huku wakijinasibu kuwa mapambano waliyoongoza ndani ya Umoja wa Ulaya yamezaa matunda.

Akizungumzia hilo waziri mkuu wa Hungary  Viktor Orban, amesema "Tunaweza kusema, bila shaka kwa staha, kwamba tumenusuru umoja ndani ya muungano. Kwa hiyo usisahau kwamba mvutano huu siyo tu ulihusu utawala wa sheria, kanuni au masuala ya kifedha, bali ulikuwa kuhusu hatma ya Umoja wa Ulaya"

Vipengele vya makubaliano haviko wazi 

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema nchi yake imefanya kazi kubwa kumaliza tofauti na wasiwasi wa Poland na Hungary kuhusiana na masharti yaliyopendekezwa bila hata hivyo kuathiri utekelezaji wake.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani Picha: Olivier Matthys/AP/picture alliance

Hata hivyo bado hakuna taarifa za kina kuhusu kila kilichokubaliwa baina ya pande mbili lakini wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wamesema masharti ya kushinikiza utawala wa sheria yatasubiri ufafanuzi wa mahakama ya Umoja wa Ulaya, mchakato utakaochukua kiasi mwaka mmoja.

Mvutano huo wa bajeti umemalizika siku  kadhaa tangu mataifa mengine wanachama 25 ya Umoja wa Ulaya kuashiria kwamba yako tayari kutengeneza mpango mwingine wa uokozi bila kuzijumuisha Hungary na Poland uamuzi ambao ungezinyima nchi hizo msaada wa mabilioni ya Euro.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW