1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBrazil

Viongozi wa G20 kujadili maendeleo na nishati safi

19 Novemba 2024

Mkutano wa kilele wa kundi la nchi tajiri na zile zinazoinukia kiuchumi la G20 unaingia siku ya pili leo ambapo viongozi waliokusanyika Brazil watajadili suala la maendeleo endelevu na matumizi ya nishati safi.

Viongozi wa mataifa wanachama wa kundi la G20 wakishiriki mkutano wa kilele mjini Rio
Viongozi wa mataifa wanachama wa kundi la G20 wakishiriki mkutano wa kilele mjini Rio. Picha: Eric Lee/The New York Times/AP/picture alliance

Katika siku ya pili ya mkutano huo wa mjini Rio viongozi wa kundi la G20 wanalenga kujadili kwa kirefu suala la maendeleo na mazingira.

Wanatumai maazimio yao yataongeza msukumo kuelekea kupatikana mkataba wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwenye mkutano mwingine mkubwa wa mazingira wa COP29 unaondelea huko Baku, Azerbajain.

Hapo jana mwenyeji wa mkutano wa COP29 alizarai nchini za G20 kutuma ujumbe madhubuti juu ya ulazima uliopo katika kushughulikia janga la mabadiliko ya tabianchi na kuyanusuru majadiliano yanayosusasa baina ya mataifa yanayokutana nchini Azerbaijan.

Wengi wanasisitiza kwamba ni muhimu kupatikane mkataba mjini Baku utakaoweka wazi dhima ya nchi tajiri katika kufadhili miradi ya kupambana na taathira za mabadiliko ya tabianchi.

Wachambuzi wasema tamko la viongozi wa G20 limepwaya kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Mkutano wa COP29 mjini Baku, Azerbaijan.Picha: Sean Gallup/Getty Images

Katika tamko lao la mwisho lililotolewa jana Jumatatu, viongozi wa G20 wamehimiza kuongezwa haraka na kwa muda mrefu utolewaji wa fedha za kupambana na balaa la kupanda kwa kiwango cha joto kwenye uso wa dunia.

Wamependekeza kiwango cha michango kifikie matrilioni ya dola na fedha hizo zitafutwe kutoka kila chanzo huku wakisisitiza kwamba mkutano wa COP29 ni sharti uoneshe jinsi nchi tajiri ziakavyotoa fedha kuyasaidia mataifa masikini kwenye miradi ya mazingira.

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wanasema lugha iliyotumika kwenye tamko hilo la viongozi wa G20 ni la "jumla jumla" na limeshindwa kuonesha ni vipi mwafaka utapatikana kwenye mkutano wa COP29.

Wachumi wanakadiria juhudi za kupambana na  mabadiliko ya hali ya hewa zinahitaji angalau dola Trilioni moja kila mwaka. Lakini nchi tajiri ikiwemo za Ulaya zinataka idadi ya wachangiaji fedha iongezwe kuzijumuisha nchi zinazoendelea lakini zenye ukwasi mkubwa kama China na madola tajiri ya Mashariki ya Kati.

Mageuzi ya Baraza la Usalama na tozo kwa matajiri yajitokeza mkutano wa G20 

Mbali ya suala hilo tamko la viongozi wa G20 liligusia kidogo vita vya Urusi na Ukraine na mzozo wa Mashariki ya Kati. Mwenyeji wa mkutano huo, Brazil, alitoa kipaumbele katika ajenda za kijamii kwenye mkutano wa mwaka huu.

Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil, mwenyeji wa mkutano wa G20.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Katika siku ya kwanza ya mkutano jana Jumatatu, Rais Luiz Inacio Lula da Silva aliwaongoza wenzake kuzindua "Mkakati wa ulimwengu wa kupambana na njaa na umasikini" akisema changamoto hizo mbili ni matokeo ya "sera mbovu za kisiasa na siyo ukosefu wa rasilimali."

Viongozi wa G20 wametoa mwito pia wa mageuzi wa taasisi za kimataifa hasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakitaka liongeze "uwakilishi, liwe na ufanisi na liwajibike" kutimiza malengo ya kuundwa kwake.

Viongozi pia wameelezea dhamira yao ya kuweka mfumo wa kimataifa wa kuwatiza kodi watu matajiri zaidi ili kukusanya fedha za kuboresha maisha ya wengine walio dhalili.

Licha ya wasiwasi uliokuwepo kabla kutokana na upinzani wa Argentina, kundi la G20 limefanikiwa kuchapisha tamko la mwisho lenye vipengele 85 na rais Lula inaonesha amefanikiwa kuziweka mbele ajenda zake kwenye mkutano wa mwaka huu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW