G7 kutoa dola bilioni 5 kukabili kitisho cha njaa
28 Juni 2022Viongozi wakuu wa nchi na serikali wa kundi la nchi tajiri kiviwanda duniani G7 wanatarajiwa kutoa ahadi ya dola bilioni tano kuimarisha usalama wa chakula duniani,miongoni mwa hatua nyingine,wakati wakikamilisha mkutano wao wa kilele unaofanyika huko Kusini mwa Ujerumani.
Hatua ya viongozi wa kundi la G7 ni jibu la wasiwasi unaojitokeza katika nchi zinazoendelea kuhusu kitisho cha kuzuka njaa kilichochochewa na vita vya Ukraine.Kadhalika viongozi hao wanashughulika kutafuta njia za kuisadia Ukraine kusafirisha nafaka zake kwa mujibu wa waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson.
Soma pia: Viongozi wa G7 waapa kuisaida Ukraine "bila kuchoka"
Tangazo hilo la waziri mkuu Johnson amelitowa leo mwanzoni mwa mkutano wa pembezoni wa pande tano na viongozi wa Ufaransa, Emmanuel Macron, Mario Draghi wa Italia, kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na rais wa Marekani Joe Biden.
Mpaka sasa Ukraine imeshindwa kusafirisha nafaka zake ikizuiwa na vizuizi vilivyowekwa na Urusi katika bandari zake za bahari nyesi,hatua ambayo imewalazimisha wasafirishaji kutumia njia za nchi kavu ambazo hazina uhakika.
Lakini pia Kundi hilo la viongozi wa nchi saba tajiri kiviwanda linakamilisha mkutano wake huo wa kilele leo Jumanne,mkutano ambao ulikuwa na nia ya kutuma ujumbe mzito wa kuonesha kujitolea kwa nchi hiyo katika kuiunga mkono Ukraine na mustakabali wake.
Lakini pia kuihakikishia Urusi kwamba italipia gharama kubwa kutokana na hatua yake ya kuivamia Ukraine na bila shaka pia kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa njaa duniani na kuonesha mshikamano katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.
Soma pia: Kongamano la G7 Elmau, Ujerumani: Je ni zaidi ya onyesho?
Kabla ya kumalizika mkutano huo viongozi hao wameungana kulaani shambulizi la Urusi dhidi ya jengo la maduka katika mji wa Kremechuk na kukiita kitendo hicho cha Urusi kuwa uhalifu wa kivita na kuahidi kwamba rais Vladmir Putin na wengine wanaohusika watabebeshwa dhamana.
Marekani imeelezwa kwamba itachangia zaidi ya nusu ya dola bilioni 5 zilizoafikiwa na kimsingi fungu hilo litatumika kusaidia juhudi za kuimarisha usalama wa chakula katika nchi 47, kuokoa maisha kupitia shughuli za moja kwa moja za msaada wa kibinadamu,pamoja na kuimarisha mifumo ya uzalishaji chakula kote duniani na hasa katika maeneo yaliyoko hatarini.
Vita vya Ukraine ambavyo hivi sasa vimeingia mwezi wake wa tano vinasababisha hali ngumu ya kusafirishwa nafaka kutoka bandari za nchi hiyo na kuchochea ongezeko kubwa la bei ya vyakula dunia nzima. Na wataalamu na mashirika ya msaada wanatahadharisha juu ya kutokea uwezekano wa baa la njaa katika baadhi ya maeneo ya Afrika.
Soma pia: Biden: Lazima tusimame pamoja dhidi ya Urusi
Viongozi wa kundi la G7,linazijumuisha Uingereza,Canada,Ufaransa,Ujerumani,Italia, Japan na Marekani wametangaza azimio la pamoja linalojumuisha hatua iliyopigwa katika mkutano wao wa kilele katika hoteli ya kifakhari ya Schloss Elmau ambapo kansela Olaf Scholz anatarajiwa kuwa na mkutano na waandishi habari.
Viongozi hao wameonesha mshikamano mbele ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na kuonekana kupiga hatua kiasi fulani kuhusu masuala kadhaa ikiwemo kupunguza utegemezi wa nishati kutoka Urusi na hatua za kuiadhibu nchi nchi hiyo pamoja na kuunga mkono juhudi za Ukraine katika vita hivyo.
Soma pia: G7 yaweka hazina ya miundombinu kwa nchi zinazostawi
Juu ya hayo afisa kutoka Ikulu ya Marekani amesema kuna uwezekano viongozi wa G7 wakawapa majukumu mawaziri wao kuanzisha mchakato wa utaratibu wa kuweka viwango maalum katika bei ya mafuta kutoka Urusi. Ingawa kwenye mkutano huo wa kilele wakosoaji walitowa hoja kwamba hatua hiyo itakuwa vigumu kuitekeleza. Viongozi wa G7 wanajaribu kuizuia Urusi kutopata faida kutokana na ongezeko la bei.