Viongozi wa Israel,Misri na UAE wakutana kwa mara ya kwanza
22 Machi 2022Rais wa Misri AbdelFatah al Sissi, waziri mkuu wa Israel Naftali Bennett pamoja na mrithi wa Ufalme wa Umoja wa Falme za Kiarabu Mohammed bin Zayed wamekutana katika eneo la kitalii la Sharm el Sheikh nchini Misri na kujadiliana kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa.
Mazungumzo yao yakilenga zaidi kuhusu utulivu wa soko la nishati pamoja na usalama wa chakula. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais wa Misri leo Jumanne.
Mtawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu Mohammed bin Zayed aliwasili Misri akiongoza ujumbe wake wa kiserikali mnamo Jumatatu na kukutana na rais Al Sisi wa Misri ambapo majadiliano yao yalituwama kwenye suala la ushirikiano baina ya nchi zao.
UAE pamoja na Saudi Arabia zimekataa kuongeza uzalishaji mafuta licha ya kutakiwa kufanya hivyo na nchi za Magharibi kufuatia kukupanda kwa bei katika soko la nishati ya mafuta ghafi hali iliyochochewa na hatua ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Waziri mkuu wa Israel Bennett nae aliwasili Misri Jumatatu kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na ofisi yake hii ikiwa ni ziara yake ya pili nchini Misri . Aliwahi kukutana na rais Al Sissi mnamo mwezi Septemba katika eneo hilo la Sharm el Sheikh.
Lakini huu ni mkutano wa kwanza wa pamoja wa viongozi hao watatu tangu Umoja wa Falme za kiarabu uliposaini makubaliano yaliyosimamiwa na Marekani ya kuanzisha ushirikiano rasmi na Israel mnamo mwaka 2020.
Mkutano huo wa Jumanne huko Misri umekuja siku chache baada ya rais wa Syria Bashar al Assad kukutana na mtawala wa UAE katika ziara yake ya kushtukiza nchini Emarati. Misri ilikuwa nchi ya kwanza ya kiarabu kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel mnamo mwaka 1979.