Viongozi wa kiafrika wamlilia Madiba
6 Desemba 2013Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Dr Dramini Nkosazana Zuma amesema kifo cha Nelson Mandela ni pigo si kwa Afrika Kusini na Afrika tu, bali kwa jamii nzima ya binadamu.
Bi Zuma amesema kuwa Mandela alikuwa alama ya mshikamano katika mapambano ya umma dhidi ya utawala dhalimu wa ubaguzi wa rangi, unyanyasaji na ukoloni, na kuitolea wito Afrika wa kukumbatia yale aliyoyathamini.
Nchini Tanzania siku tatu za maombolezo zimetangazwa kuomboleza kifo cha Nelson Mandela. Rais wa Tanzania Nelson Mandela amemtaja marehemu Mandela kuwa sauti ya ushujaa na chanzo cha hamasa, na kuongeza kuwa ni kipenzi cha watu aliyetoa mfano mwema.
Katika nchi jirani ya Kenya, rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyata amesema Mandela alikuwa kiongozi alitoa matumaini na mwenye kutoa msukumo wa maridhiano. Kenyatta amesema maisha ya Mandela yanatoa somo muhimu kuwa nguvu ya dhamira inaweza kuugeuza uhasama kuwa ushindi.
Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema ingawa Mandela ameaga dunia ataendelea kuishi mioyoni mwa wapenzi wake kwa muda mrefu. Nchini Nigeria, rais wa nchi hiyo Goodluck Jonathan amesema Mandela alitoa matumaini kwa wanyonge wanaonyanyasika kote ulimwenguni, na kuongeza kuwa itakuwa vigumu kuliziba pengo lililoachwa na shujaa huyo.
Askofu mkuu wa zamani wa kanisa la Kianglikana nchini Afrika Kusini Desmond Tutu ambaye amehutubia umati wa waumini waliohudhuria ibada maalumu ya kumkumbuka Mandela, amesema Afrika Kusini imefiwa na baba, na kusema zawadi nzuri ambayo nchi hiyo yaweza kumpa Mandela, ni kujenga jamii iliyoungana.
Mtangulizi wa Nelson Mandela kwenye wadhfa wa urais wa Afrika Kusini Fredrick W de Klerk, amesema nchi hiyo imempoteza mmoja wa waasisi wake na raia mwenye heshima ya hali ya juu.
Huko huko Afrika Kusini, aliyekuwa mkuu wa gereza alilofungiwa Mandela kwa muda mrefu kwenye kisiwa cha Robben, Christo Brand, amesema Mandela alikuwa mfungwa wake, rafiki yake, baba yake na rais wake.
Kifo cha Mandela kimeughubika mkutano wa marais wapatao 40 wanaokutana mjini Paris kuzungumzia usalama barani humo na kupelekwa kwa wanajeshi wa Ufaransa kutuliza hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Akizungumza katika mkutano huo, rais wa Jamhuri ya Kongo Sassou Ngueso amesema mkutano wenyewe unakwenda sambamba na yale aliyopigania Mandela wakati wa uhai wake, ambayo ni uhuru na amani kwa watu wa Afrika.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/dpae
Mhariri: Sekione Kitojo