1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

China yawapokea viongozi wa Afrika katika mkutano wa kilele

Sylvia Mwehozi
2 Septemba 2024

China imewapokea viongozi kadha wa Kiafrika wanaoshiriki kongamano baina ya nchi hiyo na Afrika wakati ikijaribu kuimarisha uhusiano na bara hilo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali ambako imetoa mabilioni ya mikopo.

China | Mkutano wa kilele wa China-na Afrika
Rais wa Gabon Brice Clotaire Oligui NguemaPicha: Ken Ishii/REUTERS

Beijing imesema kongamano la wiki hii kati ya China na Afrika litakuwa tukio kubwa zaidi la kidiplomasia tangu janga la Covid-19, huku zaidi ya viongozi na wajumbe kumi wakitarajiwa kuhudhuria. Miongoni mwa viongozi wa Afrika wanaohudhuria kongamano hilo ni Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ambaye aliwasili mapema leo kwa ziara ya siku nne ambayo itampeleka hadi kwenye mji wa kusini ambao ni kitovu cha teknolojia wa Shenzhen.

Soma: Viongozi wa nchi za Afrika kuhudhuria mkutano Beijing

Ramaphosa amekutana na rais wa China Xi Jinping na kumweleza kiongozi huyo kwamba anakusudia kupunguza nakisi ya kibiashara na Beijing, wakati kiongozi huyo wa China akitarajiwa kuwaomba viongozi wa Afrika kununua bidhaa zaidi za nchi yake. Matamshi ya Ramaphosa yanaashiria changamoto ambayo Xi atajaribu kuigusia wakati wa kongamano hilo ili kuwashawishi viongozi wa Afrika wanaokusanyika Beijing kununua zaidi bidhaa za China, haswa baada ya nchi hiyo kushindwa kufikia ahadi zake ilizotoa katika mkutano wa mwisho wa pande mbili mwaka 2021 wa kununua bidhaa za Kiafrika za dola bilioni 300. Rais Xi alimweleza mgeni wake Ramaphosa kwamba; Rais Xi aahidi kuisaidia Afrika kukuza viwanda vyake

Rais wa Kongo Felix Tshisekedi Picha: Tingshu Wang/REUTERS

"Urafiki kati ya China na Afrika Kusini umekita mizizi katika mapambano yetu ya pamoja ya ukombozi wa taifa, kusaidiana katika kukuza maendeleo ya taifa na ujenzi, umoja na ushirikiano katika kutafuta usawa na haki kimataifa. Kwa hiyo, napendekeza kuinua uhusiano kati ya China na Afrika Kusini kwenye ushirikiano wa kimkakati wa pande zote wa enzi mpya."

Mbali na Ramaphosa, Xi pia amekutana na rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi. China ina uwepo mkubwa nchini Kongo, ambako inanuia kutumia rasilimali nyingi za asili ikiwa ni pamoja na madini ya shaba, dhahabu, lithiamu na madini adimu duniani. Viongozi wa Djibouti ambako kunapatikana kambi ya kwanza ya kijeshi ya nje ya China pamoja na Guinea ya Ikweta, Nigeria, Mali na wengine pia wamewasili Beijing tayari kwa kongamano kubwa.Mikopo ya China kwa Afrika yapungua mwaka 2022 China imetuma mamia kwa maelfu ya wafanyakazi barani Afrika kujenga miradi yake mikubwa huku ikigusa maliasili nyingi za bara hilo yakiwemo madini.

Rais wa Afrika Kusini Cyril RamaphosaPicha: Tingshu Wang/REUTERS

Mikopo yake mikubwa imefadhili miundombinu lakini pia ilizua utata haswa kwa nchi zinazokabiliwa na mzigo wa madeni makubwa. China, ambayo inashikilia nambari mbili kwa uchumi mkubwa duniani, ni mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara barani Afrika, huku biashara kati ya pande hizo mbili ikifikia dola bilioni 167.8 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya China.Mikopo inayohusishwa na maliasili za Afrika yakosolewa

Hata hivyo mikopo ya Beijing kwa mataifa ya Afrika mwaka jana ilikuwa ya juu zaidi katika kipindi cha miaka mitano. Nchi zilizoongoza katika orodha ya wakopaji wakubwa kwa China ni Angola, Ethiopia, Misri, Nigeria na Kenya. Mkutano wa wiki hii unafanyika wakati viongozi wa Afrika wakitizama ushindani mkubwa wa mamlaka kati ya Marekani na China kuhusu rasilimali na ushawishi barani Afrika.