1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Kiarabu wamuunga mkono Mfalme Abdullah wa Jordan

4 Aprili 2021

Viongozi wa mataifa ya kadhaa ya Kiarabu na yaliyo na Waislamu wengi wamejitokeza hadharani leo kumuunga mkono Mfalme Abdallah II wa Jordan kufuatia mtikisiko wa hali ya usalama uliokhofiwa kuwa jaribio la mapinduzi.

Jordanien König Abdullah Prinz Hamzah al-Hussein 2012
Picha: Balkis Press/abaca/picture alliance

Nchi jirani ya Saudi Arabia ilisema kwamba inauunga mkono kikamilifu utawala wa Kihashimiyyah wa Jordan na pia hatua zilizochukuliwa na "Mfalme Abdullah wa Pili na Mrithi wa Kiti cha Ufalme Hussein ili kulinda usalama na utulivu."

Taarifa kama hiyo imetolewa na katibu mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, ambaye kupitia ukurasa wa Facebook, alisema jumuiya hiyo inaunga mkono moja kwa moja hatua zote za kudumisha usalama na utulivu. 

Baraza la Ushirikiano wa Mataifa ya Ghuba (GCC) nalo pia limethibitisha kuunga kwake maamuzi yote ya utawala wa Jordan. 

Mapema asubuhi ya Jumapili (Aprili 4), vyombo rasmi vya habari nchini Jordan vilionya kwamba usalama na utulivu wa nchi hiyo ni "mpaka usiopaswa kuchupwa", ikiwa ni siku moja tu baada ya maafisa kadhaa wa ngazi za juu kutiwa nguvuni, huku kaka yake Mfalme Abdullah wa Pili, aitwaye Hamzah, akiwekwa kwenye kizuizi cha nyumbani. 

Mama wa Hamzah alaani 'fitna'

Katika picha hii ya mwaka 1999, Malkia Noorn anaonekana akiwa na mwanawe, Hamzah, wakiangalia mechi ya mpira wa kikapu kati ya Jordan na Lebanon mjini Aman.Picha: Jamal Nasrallah/AFP

Mama yake Hamzah, Malkia Noor, ambaye ana asili ya Marekani, amethibitisha kuwa mwanawe yuko kwenye kizuizi hicho, huku akilaani kile alichosema ni fitina ovu. "Naomba ukweli na haki visimame kwa waathirika wote wasiokuwa na hatia wa fitina hii ovu. Mungu awabariki na kuwahifadhi," aliandika siku ya Jumapili kupitia mtandao wa Twitter.

Hata hivyo, jeshi la Jordan lilikanusha kumshikilia Mwana Mfalme Hamzah, badala yake likasema kilichofanyika hasa ni kumtaka mrithi huyo wa zamani wa kiti cha ufalme kuacha baadhi ya shughuli ambazo zingeliweza kuyumbisha utulivu na usalama wa nchi, lakini gazeti la Washington Post liliripoti kwamba kulikuwa na jaribio la kumuangusha Mfalme Abdullah wa Pili, ambaye ni ndugu wa baba mmoja wa Mwana Mfalme Hamzah.

Picha za vidio zilizotumwa mtandaoni zinaonesha kiwango kikubwa cha polisi kwenye eneo la Dabouq lililo karibu na makasri ya kifalme mjini Amman, huku Mwana Mfalme Hamzah bin Hussein akisema amezingirwa kwenye nyumba yake.

Kupitia ukanda wa vidio ambao shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) linasema liliupata kutoka kwa wakili wake, Mwana Mfalme huyo alisema marafiki zake kadhaa walikuwa wamekamatwa, walinzi wake kuondoshwa na huduma za simu na intaneti kukatwa.

Hamzah, mrithi wa ufalme aliyekiukwa

Mwana Mfalme Hamzah al-Hussein na mkewe wa pili, Basma Bani Ahmad Al-Atoum, mwaka 2012. Awali, Hamzah alimuowa Binti Mfalme Noor Hamzah, mzawa wa Uhispania.Picha: Balkis Press/abaca/picture alliance

Mwana Mfalme Hamzah, ambaye ni ndugu wa baba mmoja na Mfalme Abdullah wa Pili, alikanusha kuwa sehemu ya "njama ama kundi lolote la kihalifu", lakini akasema kuwa Ufalme huo wa Kishamiyyah "umegeuka kisima cha ufisadi, upendeleo wa kidugu na uongozi mbaya" na kwamba hakuna mtu anayeruhusiwa kuwakosoa walio kwenye mamlaka.

Gazeti rasmi la serikali, Al-Rai, lilichapisha onyo siku ya Jumapili (Aprili 4) likisema kwamba "suala la usalama na utulivu wa nchi hiyo ni mstari mwekundu ambao haupaswi kuvuukwa au hata kukaribiwa", na kwamba taarifa rasmi ya serikali ingelitolewa baadaye.

Shirika rasmi la habari la Jordan, Petra, liliwataja wasaidizi wa zamani wa familia ya kifalme akiwemo aliyekuwa mkuu wa utawala baina ya mwaka 2007 na 2008, Bassem Awadallah, pamoja na Sherif Hassan bin Zaid kuwa miongoni mwa watu wanaoshikiliwa. Likinukuu chanzo kimoja cha usalama, shirika hilo lilisema kuwa wawili hao walikamatwa kwa "kwa sababu za kiusalama".

Hamzah ana mahusiano mazuri rasmi na ndugu yake Abdullah na ni mashuhuri sana miongoni mwa makabila ya Jordan. Mfalme Abdullah alimteuwa Hamzah kuwa mrithi wa kiti cha ufalme mwaka 1999 kwa kutekeleza usia wa baba yao, lakini mwaka 2004 akamvuwa wadhifa huo na kumpa mwanawe wa kwanza wa kiume, aitwaye Hussein.
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW