1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Kiarabu wataak hatua zichukuliwe dhidi ya Iran

Sekione Kitojo
31 Mei 2019

Mfalme Salman wa Saudi Arabia ametoa wito wa kuchukuliwa hatua kali kuizuwia Iran kuendelea na uchokozi wakati wa mkutano wa dharura wa jumuiya ya mataifa ya Kiarabu ulioitishwa baada ya mashambulio katika eneo la Ghuba

Riad Treffen GCC Außenminister
Picha: Getty Images/AFP/F. Nureldine

"Kutokuwapo kwa  msimamo  mkali na  madhubuti kukabiliana na vitendo  hivi  vya  kigaidi  vya  utawala  wa  Iran katika  eneo  hili kumesababisha  Iran iendelee na hali  hiyo na  pia  kuongezeka ambako  tunakuona," Mfalme Salman  amesewaambia  viongozi  wa mataifa  ya  kiarabu.

Mfalme Sakman inb Abdul al Aziz ( kushoto) na Mfalme Mohammed wa 4 wa Morocco (kulia)

"Hivi  leo tunakabiliwa  na  kitisho  katika  usalama  wa mataifa  ya kiarabu, operesheni  za  uharibifu zinazolenga  meli  za  kibiashara karibu  na eneo  la  maji  la Umoja  wa  Falme za  Kiarabu , kushambuliwa  vituo viwili  vya  kusukuma  mafuta nchini  Saudi Arabia kulikofanywa  na  wanamgambo  magaidi wanaoungwa mkono  na  Iran.

Mapema  mwezi  huu , meli  nne za  kibiashara  zilihujumiwa  nje  ya pwani ya  Umoja  wa  Falme  za  Kiarabu UAE, na ndege zisizokuwa na  rubani  zenye  mabomu  zilishambulia  vituo  viwili  vya kusukumia  mafuta  katika  bomba la  mafuta  katika  jimbo  la  Riyadh nchini  Saudi Arabia.

Mei 18, Mfalme Salman aliitisha  mkutano  wa  dharura  wa jumuiya ya  mataifa  ya  Kiarabu  kujadili  mashambulio  hayo, ambayo Marekani  imeitwisha  jukumu  Iran, hasimu  wa  kikanda  wa  Saudi Arabia. Iran inakana  shutuma  hizo.

Viongozi wa mataifa ya Kiarabu katika picha ya pamoja kabla ya mkutano wao wa mataifa ya KiarabuPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Nabil

Taarifa ya  viongozi  wa  mataifa  ya  kiarabu  inayoshutumu Iran kwa  kuingilia  masuala  ya  mataifa  ya  kanda  hiyo yamekanushwa vikali  na  Iran leo, ambapo  msemaji  wa  wizara  ya  mambo  ya kigeni  ametupilia  mbali  shutuma  hizo  na  kusema  ni  madai yasiyo na  msingi.

Matumizi mabaya ya mwezi wa Ramadhan

Msemaji wa  wizara  ya  mambo  ya kigeni ya  Iran Abbas Mousavi ameliambia  shirika  la  habari  la  nchi  hiyo ISNA kuwa  Saudi Arabia  imetumia mwezi  wa  Ramadhani  na  mji  mtakatifu  wa Mecca kupata  manufaa  ya  kisiasa ili  kuieleza  dunia  kuhusu madai  yasiyo  na  msingi dhidi  ya  Iran. Ameongeza  kwamba  lengo kuu la  mataifa  ya  Kiislamu  na  Kiarabu  linapaswa kuwa ukombozi wa Wapalestina, na  sio  kulumbana.

Hata hivyo rais wa Iraq Barham Salih  amewataka  viongozi wa mataifa  ya  Kiarabu  kutafakari  kabla  ya  kuchukua  hatua  dhidi  ya Iran.

Saudi Arabia inailalamikia Iran kwa kuhujumu vituo vyake vya mafutaPicha: Getty Images/AFP/A. Kenare

"Ndugu zangu, katikati ya nyakati hizi tete na matukio yanayotokea kwa kasi na kanda hii yenye  hali ya wasiwasi na  mazingira  ya dunia yenye wasi  wasi  mkubwa na  vitisho, tunashuhudia  mbele ya  macho yetu kuongezeka kwa  mzozo wa  kikanda  na  kimataifa ambao unaweza  kugeuka  kuwa  vita  ambavyo vitatuhusu sisi wote. Iwapo mzozo huu  hautashughulikiwa  vizuri, tutakabiliwa  na  hatari ya makabiliano  kikanda  na  kimataifa ambayo yataleta maafa kwa nchi zetu."

Mfalme wa Saudi Arabia  amerudia leo kusema  kwamba  nchi  hiyo wakati  wote  itanyoosha  mkono kwa  ajili  ya  ushirikiano na majadiliano na  mataifa  mengine ya  kanda  hiyo na  duniani  ili kuhimiza  maendeleo na  ufanisi na  kufikia amani ya  kudumu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW