Viongozi wa dini huko Kivu ya Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameafikiana kuiunga mkono serikali katika juhudi za kusaka amani kwenye eneo hilo.
Matangazo
Eneo hilo liliwekwa chini ya utawala wa kijeshi tangu mwezi wa Mei mwaka jana. Viongozi hao wa kidini wameamua kuyatembelea maeneo yanayoathirika na vita vinavyoendeshwa na makundi ya waasi kusambaza ujumbe wa amani.
Kwa muda wa masaa matano viongozi hao kutoka dini za Kikristo na Kiislamu wamekuwa wakijadili kuhusu mikakati muafaka inayoweza kutumiwa kuhamasisha vijana kuachana na makundi ya waasi yanayoendelea kuwaua raia katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri mikao ambamo baadhi ya vijiji vimeendelea kubaki na ukiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Wily Ngumbi Ngengele, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki mjini Goma, amebainisha kuwa ushirikiano huu ni njia pekee itakayoweza kuisaidia serikali ya Kongo kudumisha amani na usalama eneo lote la mashariki mwa Congo.
Kwa muda mrefu makanisa yamekuwa yakiingilia kati maswala ya kiusalama mashariki mwa Congo lakini bila mafanikio makubwa, huku kukiendelea kushuhudiwa ongezeko la makundi ya waasi ambao asilimia kubwa ni vijana waliopoteza matumaini ya kupata ajira.
Aidha, viongozi hao wa kidini wamedai kuwa sala pamoja na nyimbo zitatumiwa katika kipindi cha miezi mitano ya kutembelea maeneo yaliyoathirika kwa vita ili kuwaweka raia wote katika hali ya kuhimiza amani.
Kwa zaidi ya miongo miwili sasa raia wanaoishi katika vijiji vya ndani pamoja na mamia ya wengine wanaoishi katika wilaya ya Beni wameendelea kuwa wahanga wa mashambulizi yanayoendeshwa na makundi ya Mai Mai, likiwemo la ADF Nalu linalowaua raia kwa kuwakata kwa mapanga.
'Laana ya rasilimali za Congo'
Madini ya Kobalti na Koltani yanapatikana kwa wingi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Lakini, kutokana na msukosuko wa kikanda, madini hayo huwavutia wapiganaji, unyanyasaji na machafuko
Picha: picture-alliance/dpa/J. Bätz
Utajiri wa rasilimali na fursa za machafuko
Katika mikoa tete ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, madini kama dhahabu na bati huyavutia makundi ya wapiganaji. Makundi hayo huwanyanyasa watu, wakiwemo watoto, kuchimba "madini ya maeneo ya migogoro'. Mapato hutumika kununua silaha ili kuyakamata maeneo zaidi na kuendeleza mapigano
Picha: picture alliance / Jürgen Bätz/dpa
Kuwalinda raia na operesheni halali za uchimbaji madini
MONUSCO, jeshi kubwa kabisa na la gharama kubwa la kulinda amani, linafanya kazi kuweka utulivu katika mikoa ya Kivu kaskazini na Kusini, ambayo ndio kitovu cha machafuko nchini humo. Vikosi vya usalama huweka doria katika vijiji vya uchimbaji madini kama Nzibora, kinachopatikana ukingoni mwa Zola Zola, chimbo halali la madini ya cassitérite
Picha: picture-alliance/dpa/J. Bätz
Kutengeneza simu za mkononi kwa gharama ya maisha ya binaadamu
Cassiterite ni moja tu ya madini yanayotumika katika simu za mkononi. Nusu ya madini hayo ulimwenguni inatoka Afrika ya Kati. Uuzaji wa bati, dhahabu na madini mengine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umekuwa chini ya uchunguzi tangu 2010, wakati sheria zilipitishwa Marekani zikihitaji orodha ya kampuni za Kimarekani kuhakikisha mauzo yao sio madini ya kutoka katika maeneo ya migogoro
Picha: picture-alliance/dpa/D. Karmann
Kuthibitisha uhalli wa madini
Picha ya tangazo kijijini Nzibira inafafanua namna vifurushi vya madini vinahitaji kufungwa vizuri na kuwekwa kibandiko na mkaguzi wa mgodi ili chanzo cha madini hayo kithibitishwe na kampuni za Marekani. Mfumo huo, hata hivyo, una mapengo mengi. Migodi haramu inaweza kuuza kwa urahisi madini kwenye soko la magendo au kufanya biashara haramu na mgodi halali ili yawekwe katika vifurushi huko
Picha: picture-alliance/dpa/J. Bätz
Unyanyasaji wa watoto
Licha ya juhudi za makundi ya haki za binaadamu, ukiukaji wa haki za binaadamu bado umekithiri katika operesheni za uchimbaji madini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Watoto kama vile Esperance Furahaare, aliyetekwa nyara na kubakwa na wapiganaji wakati akiwa na umri wa miaka 14, ni waathiriwa wa unyanyasaji na machafuko.
Picha: picture-alliance/dpa/J. Bätz
Athari za Kimazingira
Migodi, ambayo ni changamoto kwa polisi, inaweza pia kuathiri mazingira na jamii zilizo karibu. Katika migodi haramu, maji taka yanayomwagika aghalabu huishia kwenye vyanzo vya maji ya wakaazi, na kuyachafua
Picha: picture-alliance/dpa/J. Bätz
Mustakabali usiojulikana wa sheria zinazokabili madini ya maeneo ya migogoro
Wabunge wa Marekani wanajaribu kuujadili mswada ambao utayafuta mageuzi ya mwaka wa 2010. Wwanahoji Sheria ya Dodd-Frank imezuia maendeleo ya kiuchumi Marekani na haijatatua unyanyasaji Afrika ya Kati. Huku kampuni za Marekani zikihitaji kuhakikisha zinanunua madini yasiyotoka maeneo ya migogoro, kile zinachohitajika kufanya ni kuwauliza wanaowauzia, sio ushahidi wa uuzaji au yalikotoka
Picha: picture-alliance/dpa/J. Bätz
Picha 71 | 7
Haya yanajiri miezi michache tu baada ya ushirikiano wa jeshi la Kongo pamoja na Uganda kuanzisha mashambulizi makali dhidi ya ngome za waasi wa ADF Nalu katika wilaya ya Beni na kuanza kurejesha matumini ya amani kwa maelfu ya raia.