1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa kijeshi wa Guinea wavutia wawekezaji

29 Septemba 2021

Wanajeshi waliyoipindua serikali walioongozwa na Luteni Kanali Mamady Doumbouya wamewahakikishia wawekezaji wa kigeni kuwa watazingatia makubaliano yaliyopo.

Guinea Junta
Picha: Sunday Alamba/AP/picture alliance

Kwa mtazamo wa afisa anayefanya kazi na shirika moja la Urusi nchini Guinea, mapinduzi ya serikali yaliofanywa na jeshi la nchi hiyo Septemba 5, yaliyomwondoa madarakani rais Alpha Conde, hayakuathiri sekta ya madini kama vile wengi walivyofikiria. Afisa huyo amesema kila kitu kiko salama biashara inaendelea kama kawaida, ni kipindi tu cha mpito nchi hiyo inachopitia kwa sasa

Muda mfupi baada ya kuchukua madaraka, viongozi walioongoza mapinduzi hayo waliondoa mara moja marufuku zilizowekwa katika maeneo ya madini na kuhimiza makampuni kuendelea na shughuli zao na kuhakikisha migodi inabakia kuwa wazi.

Wiki moja baada ya mapinduzi hayo, Doumbouya alikutana na wakurugenzi wa madini kuwahakikishia kuwa upande huo upo salama na hapo jana jioni alitoa muongozo wa demokrasia na utawala wa kiraia nchini humo.

Kulingana na mtaalamu Paul Melly kutoka shirika moja mjini London, anaamini jeshi lililoipindua serikali limemaanisha kile ilichokisema.

"Ushahidi unaonesha wanadhamira ya kweli ya kuliongoza vizuri taifa katika kipindi cha mpito, kinachonuiwa kuwa na uongozi bora na sehemu ya hili ni kuweka mazingira bora kwa wawekezaji," alisema Paul.

Ujumbe wa ECOWAS mjini ConakryPicha: Präsidentschaft Guineas

Lakini Amadou Bah, rais wa mashirika yasio ya kiserikali yanayoshughulikia masuala ya madini, amesema jeshi hilo halina budi ila kuheshimu makubaliano ya wawekezaji maana uchumi wa Guinea unategemea asilimia 32 shughuli za madini.

Guinea ni taifa la pili duniani linalozalisha madini ya Alumini. Pia ina madini ya dhahabu na almasi na licha ya hayo nchi hiyo iliyo na idadi ya watu milini 13 ni moja ya mataifa masikini barani Afrika.

Doumbouya amesema amechukua madaraka kwa nguvu ili kumaliza tatizo hilo la umasikini na pamoja na rushwa. Sekta hiyo ya madini imekuwa ikikumbwa na rushwa ya mara kwa mara tangu Guinea ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mwaka 1958.

Luteni Kanali Mamady Doumbouya(katikati)Picha: CELLOU BINANI/AFP/ Getty Images

Kulingana na wanaharakati wa mashirika ya kiraia,  kabla ya Guinea kufaidika na utajiri wake sekta ya madini inapaswa kusafishwa kutokana na rushwa na mambo mengine yanayourejesha nyuma uchumi wa taifa hilo.

"Mikataba yote ya madini iliyotiwa saini na rais Alpha Conde ni lazima iangaliwe upya, tunajua kumekuwa na rushwa ya hali ya juu, ubadhirifu wa fedha na mambo kuendeshwa kiholela, tunasubiri kuona kile jeshi itakalofanya." walisema wanaharakati hao.

Paul Melly anasema sio mataifa ya Magharibi yatakayofaidika na Guinea kuendeshwa kidemokrasia, wawekezaji wa kuu wa taifa hilo kama Urusi na China watakuwa wakifuatilia hali kwa karibu mno.

Urusi na China hazijali sana kuhusu demokrasia ya Guinea,  ziko makini kuhakikisha hazijitengi na mataifa mengine ya Afrka Magharibi eneo ambalo zote zinajaribu kutanua ushawishi wao.

Mataifa hayo mawili kama ilivyo kwa wawekezaji wengine wanahitaji mazingira dhabiti kuendesha biashara zao. Karim Kamara mwaandishi wa habari wa DW nchini Guinea anakubaiana na hilo kwa kusema wawekezaji wanataka kujua msimamo wa jeshi likija suala la uwekezaji na wawekezaji hao wangelipenda kufanya kazi na wananchi.

Lakini iwapo sheria au kanuni zitabadilika katika sekta ya madini kuhakikisha wananchi wanafaidika  na utajiri wa taifa lao ni jambo ambalo bado litabakia kuinekana. Licha ya utajiri wa rasilimali bado Guinea itahitaji kuwa muangalifu katika biashara zake za madini.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW