Viongozi wa Korea wakutana baada ya kitisho cha Trump
26 Mei 2018Picha zilizotolewa na Korea Kusini zimemuonyesha Rais Moon Jae-in akishikana mikono na mwenzake Kim Jong Un katika upande wa Kaskazini wa ukanda usio na shughuli za kijeshi unaozitenganisha nchi hizo mbili.
Ikulu ya Korea Kusini, Blue House ilisema viongozi hao walifanya mazungumzo kwa saa mbili siku ya Jumamosi mchana katika kijiji kilekile cha mapatano cha Panmunjom, ambako walikutana mwezi uliopita, na kutoa tangazo walimoapa kuboresha uhusiano.
"Walibadilishana mawazo na kujadili njia za utekelezaji wa tangazo la Panmunjom na kuhakikisha ufanisi wa mkutano wa kilele kati ya Marekani na Korea Kaskazini," ilisema Blue House katika taarifa, na kuongeza kuwa Moon angetoa taarifa binafsi Jumapili asubuhi.
Uamuzi wa Trump ulivyoishtua Seoul
Siku ya Alhamisi Trump aliitikisa kanda hiyo kwa kufuta mkutano wake na Kim ambao ulipangwa kufanyika nchini Singapore Juni 12 akitoa sababu za "uhasama wa wazi kutoka Pyongyang."
Lakini katika muda wa saa 24 alibadilisha mwelekeo na kusema mkutano huo unaweza kuendelea baada ya mazungumzo ya tija kufanyika na maafisa wa Korea Kaskazini.
Uamuzi wa awali wa kufuta mkutano huo wa kilele wa kihistoria uliishtua Korea Kusini ambao imekuwa ikiongoza mawasiliano kati ya Washington na Pyongyang, baada ya miezi kadhaa ya kutukanana kati ya Trump na Kim pamoja na vitisho vya vita.
Picha zilizotolewa na ikulu ya Blue House pia zilimuonyesha Moon akishikana mikono na dada yake Kim, Kim Yo Jong, ambaye amekuwa na mchango mkubwa wa umma katika mazungumzo ya karibuni na Kusini, ikiwemo kuongoza ujumbe ulioshiriki michezo ya olimpiki ya majira ya baridi mwezi Februari.
Wakuu wa mashirika ya upelelezi wa mataifa yote mawili walikuwepo kwenye mkutano huo kwa mujibu wa picha hizo.
Mkutano wa nne kati ya viongozi wa Korea
Mkutano kati ya Moon na Kim umefanyika katika jengo kubwa lililoko upande wa Panmunjom wa Korea Kaskazini, kijiji chenye ulinzi mkali kilichopo kati ya mataifa hayo mawili na kinachoashiria mahala ambapo mapatano ya kusitisha vita vya Korea yalisaniwa mwaka 1953.
Mwezi uliopita viongozi hao wawili walikutano katika kijiji hicho, ambapo Kim alimualika Moon kukanyaga ardhi ya Kaskazini kabla ya wawili hao kufanya mazungumzo katika jengo lililoko upande wa Kaskazini.
Mkutano wa Jumamosi ndiyo mara ya nne kwa viongozi walioko madarakani katika Korea mbili, ambazo kimsingi bado ziko vitani, wamekutana. Tofauti na mkutano wa mwezi uliopita, uliofanyika mbele ya kamera za televisheni, mkutano wa Jumamosi ulifanyika kwa usiri wa hali ya juu, ambapo waandishi waliambiwa tu baada ya mazungumzo hayo ya ana kwa ana kukamilika.
Koh Yu-hwan, mtaalamu wa uhusiano wa Korea katika chuo kikuu cha Dongguk, alisema mkutano wa Jumamosi kati ya Moon na Kim umeongeza uwezekano wa kufanyika kwa mkutano wa kilele wa Singapore kama ilivyodhamiriwa hapo awali.
"Mkutano wa kilele wa leo unanuwia kutatua tofauti zilizosababishwa na matatizo ya kimawasiliano kati ya Washington na pyongyang na kuweka msingi wa kufanyika kwa mkutano wa kilele kati ya Marekani na Korea Kaskazini," aliliambia shirika la AFP.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri. Grace Patricia Kabogo