1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Maandamano na Waasi waafikiana nchini Sudan

26 Julai 2019

Viongozi wa maandamano nchini Sudan na washirika wao wa upande wa makundi ya waasi wamefikia makubaliano ya kumaliza tofauti kuhusu makubaliano ya kugawana madaraka na watawala wa kijeshi nchini Sudan.

Sudan Khartoum | Mohamed Hamdan Dagalo und Protestführer unterschreiben Abkommen
Picha: Getty Images/AFP/H. El-Tabei

Upande wa viongozi wa maandamano umesema siku ya Alhamisi kuwa pande zote mbili zimeahidi kufanya kazi pamoja ili kurejesha amani nchini humo.

Mnamo Julai 17 chombo kinachowakilisha vuguvugu la maandamano nchini Sudan kilitia saini makubaliano ya kugawana madaraka na watawala wa kijeshi ambayo yanaweka utaratibu wa kuundwa utawala wa mpito wa kiraia kufuatia kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir.

Lakini makundi matatu ya wapaganaji wenye silaha ambao ni sehemu ya vuguvugu la maandamano nchini humo yalipinga makubaliano hayo yakisema yameshindwa kutoa majibu kuhusu mizozo inayoendelea katika majimbo ya Darfur, Kordofan Kusini na Blue Nile.

Mazungumzo ya Addis Ababa yazaa matunda

Picha: DW/N. Dessalegn

Kutokana na tofauti hizo kundi la viongozi wa maandamano lilisafiri hadi mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa kwa mazungumzo na makundi ya waasi na baada ya siku kadhaa za majadiliano makali wamefikia makubaliano ambayo yametangazwa siku ya Alhamisi.

"Makubaliano haya yametizama kiini cha vita na yanalenga kufikia mkataba mpana wa amani na makundi yote ya wapiganaji wenye silaha” imesema sehemu ya taarifa ya Chama cha Wanataaluma wa Sudan (SPA), ambacho kiliongoza kampeni kubwa dhidi ya utawala wa Bashir.

SPA imesema azimio lililofikiwa mjini Addis Ababa linanuwia kuongeza kasi ya kuunda serikali mpya ya mpito ya kiraia kama ilivyoafikiwa kwenye makubaliano na watawala wa kijeshi.

Makundi ya waasi pia yamethibitisha kwamba tofauti zilizokuwepo na viongozi wa makundi ya waandamanaji zimetatuliwa.

"Nadhani kupitia makubaliano haya tutaungana, na kuwa imara” amesema Nuraddayim Taha, mjumbe wa kundi la waasi katika mazungumzo ya mjini Addis Ababa.

Mivutano imesababisha madhara makubwa kwa raia wa Sudan

Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Kwa miaka kadhaa sasa makundi hayo ya waasi yamekuwa yakipigana dhidi ya vikosi vya serikali kwenye majimbo ya Darfur, Kordofan Kusini na Blue Nile.

Katika mizozo hiyo mitatu makumi kwa maelfu ya watu wameuwawa na mamilioni wameyahama maskani yao, ambapo mamia kwa maelfu wanaishi katika kambi za wasio na makaazi.

Viongozi wa maandamano na majenerali wa jeshi bado hawajitoa saidi tamko la kikatiba wakisubiri kuafikia juu ya masuala muhimu ikiwemo namna haki ya waliouwawa wakati wa maandamano itakavyopatikana.

Makundi ya waasi yametaka makubaliano hayo mapya yahimize serikali mpya kuifanya amani kuwa suala la kiapumbele.

Pindi makubaliano hayo yatahitimishwa duru zimearifu kuwa makundi ya waasi yanataka nayo kuwa sehemu ya serikali ya mpito.

Wakati huo huo mamia ya raia nchini Sudan jana wameandamana kwenye mji mkuu Khartoum na kwengineko kushinikiza serikali mpya ya mpito inayotarajiwa kuundwa karibuni ihusishe wataalamu badala ya vyama vya siasa.

Hata hivyo hapajakuwa na mrejesho wowote kutoka vyama vya siasa nchini humo lakini chama cha upinzani cha Congress kiliweka vidio za maandamano hayo ya mjini Khartoum na Omdurman kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW