1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa makanisa Kongo wataja kuwepo kasoro za uchaguzi

29 Desemba 2023

Viongozi wa makanisa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo wametaja kuwepo kwa ''kasoro nyingi na udanganyifu'' katika uchaguzi wa hivi karibuni nchini humo

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki mjini Kinshasa, Kadinali Fridolin Ambongo
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki mjini Kinshasa, Kadinali Fridolin AmbongoPicha: Giscard Kusema/Presse- und Kommunikationsdienst der Präsidentschaft von Kongo

Katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Kinshasa, ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi unaosimamiwa na kanisa katoliki na kanisa la kiprotestanti nchini Kongo, uliibua maswali kuhusu uhalali wa mchakato huo wa upigaji kura.

Soma pia: Rais Tshisekedi ashinda kura za awali za jiji la Kinshasa

Mkuu wa kongamano la maaskofu wa kikatoliki nchini humo Donatien Nshole, amesema ujumbe huo umegundua visa vingi vya ukiukwaji wa taratibu za upigaji kura ambavyo huenda vikaathiri uadilifu wa matokeo ya kura mbalimbali katika maeneo tofauti.

Kurefushwa kwa uchaguzi ni kinyume cha sheria

Katika mkutano na waandishi wa habari, Nshole ameitaka tume ya uchaguzi nchini humo CENI kutangaza matokeo hayo ya awali kwa kuzingatia kituo kwa kituo.

Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo Felix TshisekediPicha: Giscard Kusema/Presse- und Kommunikationsdienst der Präsidentschaft von Kongo

Katika ripoti ya awali iliyotolewa jana Alhamisi, ujumbe huo wa waangalizi umesema kwamba kurefusha rasmi uchaguzi huo kwa siku moja ni kinyume cha sheria za uchaguzi.

Kulingana na ujumbe huo, baadhi ya watu walikuwa bado wanapiga kura kufikia Desemba 27, na umeitaka tume ya uchaguzi kufafanua hali ya kura hizo.

Hadi usiku wa kuamkia jana Alhamisi, tume ya uchaguzi , ilitangaza matokeo ya kura zaidi ya milioni 9 ambazo tayari zimehisabiwa.

Soma pia:Wagombea wa upinzani Kongo wanapanga maandamano ya kupinga uchaguzi wa rais

Rais Felix Tshisekedi anayewania muhula wa pili ameonekana kupata kura zaidi ya milioni saba ambazo ni sawa na asilimia 77, mpinzani wake wa karibu Moise Katumbi akiwa na asilimia 15 na Martin Fayulu akishika nafasi ya tatu kwa asilimia 4 pekee.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW