Viongozi wa mataifa ya kusini mashariki mwa Asia wakutana
22 Juni 2019Wakati vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vikigubika muonekano wa uchumi wa mataifa hayo unaoongozwa na biashara ya mauzo ya nje.
Mizozo katika eneo tete la bahari ya kusini mwa China, uteswaji wa Waislamu wa Rohingya na Myanmar na uchafuzi wa taka za plastiki katika bahari pia ni masuala yanayopangwa kujadiliwa katika mkutano huo wa siku mbili wa Umoja wa mataifa ya kusini mashariki mwa Asia, ASEAN, chini ya uenyekiti wa Thailand.
Lakini biashara itachukua nafasi ya kati katika mkutano huo wa viongozi wa ASEAN ambao wana nia ya kuharakisha kutiwa saini kwa makubaliano ya kibiashara yaliyotayarishwa na China yanayowafikia karibu nusu ya wakaazi wote wa dunia.
Makubaliano hayo yanayofahamika kama Ushirikiano mpana wa kiuchumi wa kimkoa RCEP , unajumuisha mataifa yote 10 ya Umoja wa ASEAN, pamoja na India, Japan, Korea kusini , Australia na New Zealand.
Yanaonekana kuwa ni utaratibu wa China kuandika sheria ya biashara kwa mataifa ya Asia na Pacifiki, kufuatia Marekani kujitoa kutoka katika eneo hilo.
Kuwekeana ushuru kwa kulipiza
Muda mfupi baada ya kuchaguliwa rais Donald Trump aliiondoa Marekani kutoka ushirikiano huo wa eneo la bahari ya Pacifiki , TPP, ambao ungekuwa ni makubaliano makubwa kabisa ya biashara duniani, akiushutumu kuwa unauwa ajira nchini Marekani.
Wakati hatua za kulipizana kwa kuwekeana ushuru wa juu kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani zimeshuhudia baadhi ya makampuni yakiikimbia China na kukimbilia katika maeneo mengine ya salama katika mataifa ya ASEAN, wataalamu wa uchumi wanasema picha pana zaidi kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wa dunia inatia shaka.
Katika muktadha huo, RCEP ni muhimu kwa kuongeza kiwango cha biashara," msemaji wa serikali ya Thailand Wrrachon Sukhondhapatipak aliwaambia waandishi habari.
"Ni bora zaidi iwapo makubaliano ya RCEP yataanza kazi haraka," Martin M. Andanar , waziri wa mawasiliano wa Ufilipino amewaambia waandishi habari.
"Biashara huru ni kitu bila shaka tunachokihitaji katika kanda hii," amesema , na kuongeza kuwa mzozo wa kibiashara kati ya China na Marekani umesababisha , "duniani nzima kupata homa".
Hatua za maendeleo zimesita sita katika miezi ya hivi karibuni wakati India ikiweka munda kutokana na hofu ya bidhaa za bei ya chini za China kuingia na kufurika katika soko hilo kubwa la nchi hiyo.
Australia na New Zealand pia zimeonesha wasi wasi kuhusiana na ukosefu wa usaalma wa kazi na mazingira.