1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMalta

Nchi za Umoja wa Ulaya zajadili juu ya swala la uhamiaji

29 Septemba 2023

Viongozi wa nchi tisa zilizo kwenye Bahari ya Mediterania na za kusini mwa Ulaya wanakutana Malta pamoja na Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen. Wanajadili kuhusu uhamiaji na masuala mengine.

Symbolbild | Ocean Viking rettet Migranten
Picha: Valeria Ferraro/AA/picture alliance

Mataifa yanayowakilishwa katika mkutano huo wa siku moja ni pamoja na mwenyeji Malta, Ufaransa, Ugiriki, Italia, Croatia, Cyprus, Ureno, Slovenia na Uhispania. Slovenia na Croatia, ambazo zipo kwenye ukanda wa pwani ya Bahari ya Adriatic, ziliongezwa kwenye kundi hilo la nchi za Mediterania mnamo mwaka 2021.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya, Ursula von der LeyenPicha: Jean-Francois Badias/AP Photo/picture alliance

Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya, Ursula von der Leyen na Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel ni miongoni mwa viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya wanaohudhuria mkutano huo wa faragha.

Viongozi wa mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya wanafanya mkutano huo usio rasmi wa Baraza la Ulaya ambao umepangiwa kufanyika wiki ijayo huko Granada, Uhispania.

Soma pia:Uhamiaji Umoja wa Ulaya bado suala tete

Viongozi hao wa nchi wanachama wa jumuiya ya Umoja wa Ulaya wanajadili juu ya changamoto zinazokabili nchi zao ambazo zinafanana kama vile uhamiaji, usimamizi wa Umoja wa Ulaya suala ambalo limeleta mijadala mingi ya kitaifa kwenye serikali za nchi za Ulaya kwa miaka mingi.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema katika mkutano huo, watajadili mambo muhimu juu ya mustakabali wa eneo la Mediterania na amesema hakuna mahala pazuri pa kufanya majadiliano hayo kuliko Malta, ambako ni kwenye njia panda baina ya Ulaya, Afrika na eneo la Mashariki ya Kati.

Rais wa Baraza la Ulaya, Charles MichelPicha: Sajjad Hussain/AFP/Getty Images

Mkutano huo unafanyika siku moja baada ya mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi za Umoja wa Ulaya kuangazia sheria mpya za jinsi jumuiya hiyo inavyowashughulikia watu wanaotafuta hifadhi na wahamiaji wasio wa kawaida.

Umoja wa Ulaya uko tayari kufikia makubaliano ya mkataba ulioboreshwa kuhusu wahamiaji na wakimbizi, ambao unalenga kupunguza shinikizo kwa nchi zilizo kwenye mstari wa mbele kama vile Italia na Ugiriki. Mkataba huo unazingatia juu ya kuwahamisha baadhi ya wahamiaji na kuwapeleka katika mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya.

Poland na Hungary nchi zinazopinga kuwakaribisha wanaotafuta hifadhi na nchi nyingine kama hizo zitahitajika kuzilipa nchi zinazowachukua wahamiaji.

Maafisa wamesema wanatarajia makubaliano kufikiwa katika siku zijazo, ingawa Italia imeomba muda zaidi wa kupitia nakala iliyotolewa.

Soma pia:Mwaziri wa Uhamiaji wakutana Brussels kujadili mustakabali wa waomba hifadhi

Kamishna wa masuala ya ndani wa Umoja wa Ulaya Ylva Johansson, alisema jana Jumatano baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya kwamba kutoelewana ndani ya kambi hiyo ya mataifa 27 kuhusu marekebisho yaliyopendekezwa sasa kumetatuliwa kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo, kuna msukumo mpya wa kuyafikia makubaliano hasa baada ya kuongezeka kasi ya wahamiaji wanaowasili kwenye kisiwa kidogo cha Italia cha Lampedusa mapema mwezi huu.

Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni,Picha: Valeria Ferraro/AA/picture alliance

Serikali ya mseto ya Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, iliyoingia madarakani mwaka mmoja uliopita kwa ahadi ya kupinga wahamiaji, imetofautiana na Ufaransa na Ujerumani huku akizishinikiza nchi nyingine za Umoja wa Ulaya zishiriki katika kuubeba mzigo huo.

Kulingana na serikali ya Italia, kufikia mwezi wa tisa 2023, idadi ya wahamiaji waliowasili nchini Italia ilipindukia hadi wahamiaji 133,000, hiyo karibu mara mbili ya idadi ya wahamiaji waliofika Italia katika kipindi kama hicho 2022.

Vyanzo: AP/AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW