1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Olaf Scholz akutana na viongozi wa mataifa Nordic

13 Mei 2024

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umesababisha wasiwasi mkubwa miongoni mwa mataifa jirani washirika wa Ukraine ikiwemo yale wanachama wa jumuiya kujihami ya NATO.

Schweden Stockholm | Olaf Scholz in Schweden
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz yuko ziarani nchini Sweden ambako anafanya mazungumzo na waziri mkuu wa nchi hiyo Ulf Kristersson pamoja na viongozi wa mataifa mengine ya Ukanda wa Nordic.

Miongoni mwa masuala yanayojadiliwa ni pamoja na kitisho cha usalama kutoka Urusi kufuatia uvamizi wake Ukraine.

Waziri mkuu wa Sweden Ulf Kristersson amesema ushirikiano baina ya mataifa ya Ukanda wa Nordic na yale ya Baltic hivi sasa umekuwa mkubwa kuliko wakati mwingine wowote kutokana na kuongezeka vitisho vinavyosababishwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Serikali ya Sweden imesema kwenye taarifa kwamba mkutano wa siku mbili unaofanyika kati ya Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na viongozi wenzake wa mataifa ya Nordic utajadili masuala kadhaa yanayohusu sera ya usalama na hali ya usalama barani Ulaya, ikiwemo vitisho vya kijeshi na visivyokuwa vya kijeshi,hatua ya kuwaandaa raia pamoja na kuweka mifumo ya  teknolojia za kisasa.

Kitisho cha usalama ni miongoni mwa ajenda za mkutano wa siku mbili

Mazoezi ya kijeshi ya NATO-FinnlandPicha: Jonathan Nackstrand/AFP/Getty Images

Mkutano huo pia unajadili ushindani wa kibiashara baina ya pande hizo mbili.Mkutano huu unafanyika katika wakati ambapo wanajeshi wa Urusi wameanzisha operesheni ya ardhini dhidi ya eneo la kaskazini Mashariki mwa Ukraine la Kharkiv wakati Ukraine ikiwa inajikuta  katikati ya hali ngumu inayotokana na kucheleweshwa kwa msaada na nchi za Magharibi.

Na hata waziri mkuu wa Sweden Ulf Krisstersson amesema sera ya usalama na mkutano wa kilele wa Jumuiya ya kujihami NATO ndiyo masuala yatakayochukuwa nafasi kubwa ya mkutano wa leo na kesho kati yake na Kansela Scholz pamoja na mawaziri wakuu kutoka Denmark, Norway, Finland na Iceland.

Mataifa ya Nordic, pamoja na Ujerumani ni miongoni mwa wafadhili wakubwa wa Ukraine tangu nchi hiyo ilipovamiwa na Urusi mnamo mwaka 2022.

Ujerumani peke yake ni nchi ya pili duniani inayotowa mchango mkubwa kwa Ukraine ambapo hadi sasa imeshatowa Euro bilioni 14.5 kwa nchi huyo kwa mujibu wa taasisi ya Kiel.Sweden ilijiunga na muungano huo wa kijeshi wa NATO mwezi March wakati Finland ikiwa imejiunga mwezi Aprili mwaka 2023.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius Kushoto na mwenzake wa Norway Bjørn Arild GramPicha: Heiko Junge/NTB Scanpix/AP/picture alliance

Kutanuka kwa Jumuiya hiyo ni pigo kubwa kwa rais wa Urusi Vladmir Putin  historia ikionesha kujirudia kwa hali iliyotokea barani Ulaya baada ya  vita baridi katika mtazamo mzima wa suala la usalama,uliyosababishwa na  uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Hivi sasa bahari ya Baltic kwa kiasi kikubwa imezunguukwa na mataifa wanachama wa Jumuiya ya NATO, Jumuiya hiyo ikijiimarisha kimkakati katika eneo muhimu kabisa.

Wakati mkutano huo wa Stolkholm ukiendelea huko Vilnius nako waziri mkuu wa Lithuania Ingrida Imonyte amewapokea viongozi wenzake wa Estonia,Kajja Kallas na Evika Silina,waziri mkuu wa Latvia katika mkutano wa baraza la viongozi wa mataifa ya Baltic.

Waziri mkuu wa Estonia Kallas amesema Urusi imeismarisha vita vya chini kwa chini dhidi ya mataifa ya Ulaya na kwamba inataka hasa kuyatia khofu mataifa hayo ili kuyazuia kutoisadia Ukraine.Mataifa hayo ya Baltic nayo ni waungaji mkono wakubwa wa Ukraine.  

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW