Viongozi wa Nordic wataka kuisadia zaidi Ukraine kivita
14 Mei 2024Scholz ambaye yuko ziarani Sweden jana alikuwa na mazungumzo na viongozi wa mataifa ya Ukanda wa Nordic ambapo aliyatolea mwito mataifa ya Ulaya kuiongezea msaada wa kijeshi Ukraine na hasa mifumo ya ulinzi wa anga, katika wakati nchi hiyo ikipambana kuyakabili mashambulizi ya Urusi katika eneo lake la Kaskazini Mashariki. Kansela Scholz amezisifu pia Finnland na Sweden kwa kujiunga na jumuiya ya NATO, Zaidi alisema "Kuna tofauti moja kubwa kati ya sasa na mara ya mwisho nilipohudhuria kikao kama hichi. Hivi sasa sote ni washirika ndani ya jumuiya ya NATO kama ilivyokwishatajwa. Hii imesababishwa moja kwa moja na uchokozi wa Urusi dhidi ya Ukraine na kurudi kwa ubeberu wa Urusi barani Ulaya.Uanachama wa Finnland na Sweden katika muungano wa NATO unauimarisha muungano huo na ni mafanikio kwa usalama wetu sote". KanselaOlaf Scholz na mawaziri wakuu wa mataifa ya Ukanda wa Nordic, Sweden,Denmark,Finland,Iceland na Norway katika mazungumzo yao mjini Stolkholm, walikubaliana kuongeza msaada wa silaha kuisaidia Ukraine.