1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaItaly

Viongozi wa Mediterania wakutana kujadili juu ya wahamiaji

29 Septemba 2023

Viongozi wa nchi tisa za Mediterania na kusini mwa Ulaya, akiwemo Rais Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, wanakutana leo nchini Malta kwa mazungumzo yatakayojikita juu ya suala la wahamiaji.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wa EU mjini Brussels
Viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wa EU mjini BrusselsPicha: Petr Kupec/CTK Photo/imago images

Mkutano huo unafanyika siku moja tu baada ya shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi la UNHCR kusema kwamba zaidi ya wahamiaji 2,500 wamepoteza maisha au hawajulikani waliko wakati walipokuwa wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania mwaka huu - idadi hiyo ikiwa juu zaidi ikilinganishwa na kipindi sawa na hicho mwaka 2022.

Mkutano huo wa Malta unajiri pia wakati mawaziri wa mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya wanakaribia kuafikiana juu ya pendekezo la sheria mpya ya jinsi Umoja huo utakavyoshughulikia suala la waomba hifadhi na wahamiaji, huku makubaliano juu ya hilo yakitarajiwa kufikiwa katika siku zijazo.

Kumekuwepo na msukumo mpya wa kufikia makubaliano juu ya pendekezo la sheria hizo mpya hasa kufuatia ongezeko la wahamiaji katika kisiwa kidogo cha Italia cha Lampedusa mapema mwezi huu.

Serikali ya Meloni inayoegemea siasa za mrengo mkali wa kulia, iliyochaguliwa kutokana na sera yake ya kupinga wahamiaji, imevutana na Ujerumani na Ufaransa huku Meloni akishinikiza nchi nyengine za Umoja wa Ulaya kugawanya mzigo wa kuwahudumia wahamiaji.

Hadi kufikia sasa, idadi ya wahamiaji waliowasili katika kisiwa cha Lampedusa imepindukia 133,000.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW