1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa NATO, EU wazuru Uturuki

Admin.WagnerD9 Septemba 2016

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg na Kamishna wa Mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini wameizuru Uturuki kwa mara ya kwanza tangu jaribio la mapinduzi lililoshindwa Julai 15.

Türkei Jens Stoltenberg und Fikri Isik
Picha: picture alliance/abaca/O. Yurdakadim

Awali maafisa wa Uturuki waliwatuhumu washirika wao wa Magharibi kwa kushindwa kuonyesha mshikamano kwa kuitembelea nchi hiyo baada ya jaribio la baadhi ya wanajeshi kutaka kutwaa madaraka kwa nguvu, ambamo zaidi ya watu 260 waliuawa.

NATO na Umoja wa Ulaya walilaani haraka jaribio hilo la mapinduzi, lakini pia waliionya Uturuki kuheshimu maadili ya kidemokrasia wakati wa ukandamizaji dhidi ya watumishi wa kijeshi na umma ambao umehusisha kukamatwa kwa maelfu ya watu.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akisalimiana na katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg mjini Ankara.Picha: picture-alliance/AA/Turkish Presidency/Y. Bulbul

Stoltenberg alisema baada ya kukutana na rais Recep Tayyip Erdogan siku ya Ahamisi, kwamba shambulizi dhidi ya demokrasia katika moja ya mataifa wanachama wake ni shambulizi dhidi ya misingi ya muungano huo wa kijeshi.

Uturuki ambayo ni mmoja wa wanachama 28 wa jumuiya ya NATO na ambayo imeomba kwa muda mrefu kujiunga na Umoja wa Ulaya, inatoa mchango mkubwa katika masuala ya kikanda, ukiwemo mgogoro nchini Syria - ambako hivi karibuni ilianzisha mashambulizi ya ardhini, na pia katika wimbi la wakimbizi wanaoingia barani Ulaya ambao wamesababishwa kwa sehemu kubwa zaidi na vita vya nchini Syria.

EU, Uturuki waanza kujongeleana tena

Mwanadiplomasia wa juu kabisaa wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini, alizuru mjini Ankara siku ya Ijumaa pamoja na Kamishna wa sera ya ujirani ya Umoja wa Ulaya Johannes Hahn, alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu na waziri wa masuala ya Ulaya Omer Celik.

"Tumeijadili pia Syria. Kwa ufupi kabisaa: Tumekubaliana kwamba hakuwezi kuwapo na suluhu ya kijeshi nchini Syria, kwamba suluhu ya kisiasa pekee na serikali ya mpito ndiyo vinaweza kuleta amani nchini humo. Tumekubaliana kushirikiana kujaribu kufikia usitishaji mapigano katika siku za usoni," alisema Mogerini baada ya mkutano huo.

Mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini na ujumbe wake katika mkutano na waziri wa Mambo ya kigeni wa Uturuki Mevlut Cavusoglu mjini Ankara.Picha: picture-alliance/AA/F. Aktas

Uturuki yatoa mapendekezo mbadala

Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Uturuki amesema anaamini Uturuki na Umoja wa Ulaya wanaweza kufikia muafaka juu ya kuwaruhusu raia wa Uturuki kusafiri katika Umoja wa Ulaya bila viza.

Mevlut Cavusoglu amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba Uturuki imetoa mapendekezo mbadala na maelewano kati ya Ankara na Brussels yalikuwa yanaaza kujitokeza.

Uturuki imekuwa ikitaka kujiunga na Umoja wa Ulaya kwa muda mrefu, lakini imewatuhumu wazungu kwa kukwamisha mchakato huo kwa sababu ya chuki dhidi ya taifa hilo la Kiislamu. Maafisa wa Umoja wa Ulaya wanasema Uturuki bado haijatimiza masharti kuhusu haki za msingi na uhuru.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,dpae,afpe
Mhariri: Saumu Yusuf