1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa NATO, G7 na EU kujadili uvamizi wa Urusi

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
24 Machi 2022

Rais wa marekani Joe Biden na viongozi kutoka nchi wanachama wa muungano wa kijeshi wa NATO wanakutana kwa kikao kitakachoujadili uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Belgien | Nato-Sondergipfel zum Ukraine-Konflikt
Picha: Eric Lalmand/BELGA/dpa/picture alliance

Rais wa Marekani Joe Biden na viongozi wa nchi za magharibi wanashiriki kwenye mkutano wa kwanza kati ya mikutano mitatu ya kilele inayoangazia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Mikutano hiyo inafanyika mjini Brussels, Ubelgiji. Imeandaliwa na mashirika ya NATO, Umoja wa Ulaya na kundi la G7.

Katibu mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: Benoit Doppagne/BELGA/dpa/picture alliance

Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema viongozi wa muungano huo wa kijeshi unaoongozwa na Marekani kwenye mkutano wao watashughulikia suala la uhitaji wa kuweka upya mkakati wa muda mrefu wa ulinzi kwa nchi wanachama, kwanza kwa kukubaliana kupelekwa kwa wanajeshi zaidi katika nchi wanachama za ulaya mashariki ambazo ni Romania, Hungary, Slovakia na Bulgaria.

Jumuia ya Kujihami ya NATO tayari imeshawapeleka maelfu ya wanajeshi katika nchi wanachama wa upande wa Ulaya Mashariki baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine kwa ajili ya kukabiliana na kitisho endapo mzozo utaingia katika nchi wanachama wa NATO.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky,Picha: Ukrainian Presidential Office/ABACA/picture alliance

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambaye nchi yake haiko katika muungano huo wa NATO, anatazamiwa kutoa hotuba kwa njia ya video kwenye mkutano huo na anapanga kuomba silaha zaidi na kuzishawishi nchi hizo za magharibi kuuingilia kati mzozo kati yake na Urusi kwa kuchukua hatua kali zaidi.

Kabla ya mikutano ya kilele ya mashirika yote matatu ya NATO, Umoja wa Ulaya na kundi la nchi zilizoendelea kiviwanda G7 huko mjini Brussels, Zelensky amesema nchi yake inasubiri hatua za maana kutoka kwa viongozi wa Magharibi.

Soma:Ukraine yasema jeshi lake laendelea kusimama imara kuilinda nchi

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema vikwazo zaidi vinaweza kuwekwa pamoja na kumzuia Rais Vladimir Putin kutumia hifadhi ya dhahabu ya Urusi. Johnson amesema Putin tayari amevuka mipaka na kwamba anapaswa kufikishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.

Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Mikhail Klimentyev/Sputnik Kremlin/AP Photo/picture alliance

Nchi za Magharibi zimeweka vikwazo dhidi ya mali za benki kuu ya Urusi zenye thamani ya dola bilioni 640 na pia benki kadhaa za Urusi zimezuiwa kushiriki kwenye mfumo wa malipo ya benki wa kimataifa SWIFT hali iliyosababisha kuporomoka thamani ya sarafu ya Urusi.

Vyanzo: RTRE/AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW