Viongozi wa Afrika kukutana na rais Zelensky kisha na Putin.
16 Juni 2023Viongozi hao wa nchi za Afrika wameanza juhudi zao za kusuluhisha ambapo watakutana na marais wa Ukraine na Urusi kila mmoja peke yake. Ujumbe huo wa viongozi wa Afrika unaongozwa na marais wa Afrika kusini Cyril Ramaphosa, na Macky Sall wa Senegal.
Kwa mujibu wa taarifa, rais Ramaphosa na wajumbe wenzake wameshawasili nchini Ukraine kwa ajili ya mazungumzo na rais Volodymyr Zelensky yatakayofanyika leo Ijumaa. Wajumbe hao pia wanatarajiwa kukutana na rais Vladimir Putin wa Urusi hapo kesho Jumamosi mjini St Petersburg.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kwamba viongozi wa Afrika watapendekeza hatua za kujenga hali ya kuaminiana ili kuleta amani. Kwa mujibu wa mswada wa siri ulioonekana na shirika Habari la Reuters, hatua hizo ni pamoja na Urusi kuyarudisha majeshi yake nyuma, kuziondoa silaha zake za nyuklia kutoka Belarus na kuiweka kando, hati ya mahakama ya kimataifa, ICC ya kukamatwa kwa rais Putin. Hatua nyingine ni kuondolewa kwa vikwazo.
Soma:Afika inahitaji kuendeleza mpango wa usafirishaji nafaka
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema anatumai yatapatikana mafaniko katika mazungumzo kati ya Rais wa Urusi Vladimir Putin na viongozi wa Afrika hasa juu ya mustakabali wa makubaliano ya kuruhusu usafirishaji salama wa nafaka kutoka Ukraine na pia katika juhudi kuhusu usafirishaji wa chakula na mbolea kutoka Urusi kupitia kwenye Bahari Nyeusi.
Mswada huo wa amani unaopendekezwa na viongozi wa Afrika unajumuisha mapatano juu ya usafirishaji wa ngano na mbolea bila ya masharti. Nchi za Afrika ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa sana na vita vya Ukraine ambavyo vimetatiza usambazaji wa nafaka, vyakula na vifaa vingine. Vita hivyo vimesababisha mfumuko wa bei za vyakula hali inayozorotesha zaidi maeneo yanayokumbwa na migogoro na inahatarisha kutokea baa la njaa katika baadhi ya maeneo barani humo.
Soma:Ujumbe wa Afrika katika vita vya Ukraine kuanza mwezi huu
Marais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, Macky Sall wa Senegal, Hakainde Hichilema wa Zambia, pamoja na Rais wa Comoro Azali Assoumani, ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika wakitokea nchini Poland walisafiri kwa treni kuelekea Kyiv kwa mazungumzo na rais Volodymyr Zelensky na hapo kesho Jumamosi wataelekea nchini Urusi kwa mazungumzo na rais Vladimir Putin.
Viongozi watatu rais wa Uganda Yoweri Museveni, Abdel Fattah al-Sisi wa Misri na Rais wa Congo-Brazzaville Denis Sassou Nguesso hawamo katika safari hiyo kutokana na sababu mbalimbali kinyume na ilivyopangwa hapo awali lakini wanawakilishwa.
Vyanzo: RTRE/AFP