1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika kutafuta mikakati ya kupambana na ugaidi

Zainab Aziz Mhariri: Chilumba Rashid
28 Mei 2022

Viongozi wa Afrika wanahudhuria siku ya pili leo mkutano wa kilele mjini Malabo kwa lengo la kuchangisha fedha za kushughulikia mizozo, Hii leo watajadili masuala ya ugaidi na mabadiliko yasiyo ya kikatiba,

Rais wa Senegal Macky Sall ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Afrika
Rais wa Senegal Macky Sall ambaye pia ni Rais wa Umoja wa AfrikaPicha: John Thys/AFP

Kwenye kikao hicho cha leo juu ya ugaidi viongozi wa Umoja wa Afrika watatathmini hatari zinazoendelea juu ya ugaidi na kutafuta mikakati ya kupambana na hatari hizo. Pia wataangalia namna ya kuimarisha mikakati ya pamoja dhidi ya ugaidi.

Wajumbe kwenye mkutano wa kilele wa nchi za Umoja wa AfrfikaPicha: Minasse Wondimu Hailu/AA/picture alliance

Wakuu wa nchi na viongozi wa serikali wa Umoja wa Afrika pia watajadili mapendekezo yaliyomo katika tamko la Accra juu ya mabadiliko ya serikali yanayofanyika kinyume cha katiba. Pamoja na hayo viongozi wa Umoja wa Afrika watazungumzia juhudi zenye lengo la kukomesha matukio hayo hasi barani Afrika ambayo yamekuwa yanaongezeka kwenye nchi kadhaa na hasa za Afrika magharibi.

Wajumbe kwenye kikao hicho maalumu pia watazingatia changamoto za migogoro ya kibinadamu  zinazolikabili bara la Afrika zilizothibitika kuwa kubwa zaidi kutokana na athari za kijamii na kiuchumi na athari zilizotokana na maambukizi ya virusi vya corona.  Kulingana na mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat, Waafrika wapatao milioni 113 wanahitaji misaada ya haraka mnamo mwaka huu,wakiwemo wahamiaji milioni 48, wanaotafuta hifadhi katika mataifa mengine na vilevile wakimbizi wa ndani.

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat Picha: Monasse Thierry/ANDBZ/ABACA/picture alliance

Kwenye Mkutano wao huo wa pili wa kilele, viongozi wa Afrika watajadili pia hali ya machafuko yanayosababishwa na makundi ya itikadi kali katika nchi za Libya, Msumbiji, Somalia, kanda ya Sahel, magharibi mwa Ziwa Chad na katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Umoja wa Afrika umesema katika taarifa  nchi 15 ambazo zimeathiriwa mno zinahitaji misaada ya haraka hasa wakati huu ambao athari za mabadiliko ya tabia nchi zinafanya mahitaji ya kibinadamu kuongezeka kwa kiwango kikubwa. Umoja huo umetilia maanani kuwa miongoni mwa watu milioni 30 waliopoteza makaazi yao, zaidi ya milioni 10 ni Watoto wenye umri wa chini ya miaka 15. Hali hiyo inasababishwa na mizozo ya kikabila na tatizo la upatikanaji wa chakula usiokuwa wa uhakika.

Ukame ndio chanzo cha ukosefu wa chakula barani AfrikaPicha: Mohamed Babiker/picture alliance/Photoshot

Shirika la Chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, limesema takriban watu milioni 282 miongoni mwa idadi jumla ya watu barani Afrika Bilioni 1.4, hawapati chakula cha kutosha. Hilo ni ongezeko la watu milioni 49 tangu mwaka 2019.

Chanzo:AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW