1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Palestina wataka Israel kutotambuliwa

16 Januari 2018

Viongozi wa chama cha Ukombozi wa Palestina PLO, wametoa wito wa kusitisha kuitambua Israel, katika hatua inayoweza kuwa na athari kubwa

Palästina Israel Konflikt Versammlung PLO in Ramallah Mahmoud Abbas
Picha: Getty Images/AFP/A. Momani

Viongozi walikutana kutoa jawabu kwa hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel. Ingawa hatua ya PLO inaweza kusababisha upinzani wa kimataifa, haikuwa wazi kama inafungamanisha kisheria.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu jioni mwenyekiti wa Kamati Kuu ya chama hicho cha ukombozi wa Palestina Salim Zanoun, ameitaka kamati ya utendaji ya chama hicho, ambayo ndiyo kamati ya juu zaidi ya utendaji ya Palestina, kutekeleza uamuzi huo wa kutotambuliwa kwa Israel. "Pili, tunaipa jukumu kamati ya utendaji kusitisha utambuzi wa Israel hadi itakapoitambua Palestina kama taifa kwa kufuata mipaka ya mwaka 1967. Tatu Kamati Kuu itaufufua uamuzi wake wa kusimamisha mikakati yote ya ushirikiano wa kiusalama na Israel."

Haijajulikana wazi iwapo Rais wa Palestina Mahmoud Abbad ataukubali uamuzi huo wa Kamati Kuu kwa kuwa mwaka 2015 alikataa matakwa ya kamati hiyo kufutiliwa mbali ushirikiano wa kiusalama na Israel.

Chama hicho cha ukombozi wa Palestina kilikuwa kinakutana Ramallah kutangaza mkakati kufuatia hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump kuitambua Jerusalem kama Mji Mkuu wa Israel. PLO imeitambua Israel kama sehemu ya mkataba wa Oslo wa 1993 uliotoa nafasi ya kuanzishwa kwa serikali ya utawala wa Palestina.

Kulikuwa na maandamano kuipinga hatua ya TrumpPicha: picture-alliance/Zumapress/D. Husni

Mwenyekiti Salim Zanoun amesema kwamba Marekani imepoteza uwezo wake kama mpatanishi. "Tunalaani na kukataa kabisa uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump kuitambua Jerusalem kama Mji Mkuu wa Israel na kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem. Baraza hili limeona kwamba Marekani imepoteza uwezo wake wa kuwa mpatanishi na mfadhili wa mchakato huu. Marekani haitokuwa tena mshirika katika mchakato huu hadi pale uamuzi wa Rais Trump kuhusiana na Jerusalem utakapofutiliwa mbali."

Jumapili alipokuwa akiufungua mkutano huo, Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas ambaye alipigia kura kutotambuliwa kwa Israel, aliziita juhudi za amani za Trump kama "kofi la karne."

Viongozi wa Israel wameilaani hotuba hiyo ya Rais Abbas ambaye alimshambulia Rais Trump. Katika ziara yake nchini India, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesema Rais Abbas amejitokeza waziwazi na kusema kile alichokiita "ukweli."

Waziri wa Ulinzi wa Israel Avigdor Lieberman amesema Abbas amerukwa na akili na amekata tamaa ya mazungumzo ya amani na sasa anataka makabiliano ya wazi na Israel na Marekani.

Waziri wa elimu wa Israel Naftali Bennett yeye amesema kwamba hotuba hiyo ya Abbas ni ishara ya kuelekea ukingoni kwa uongozi wake.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/APE/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW