1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

viongozi wa SADC kukutana kuhusu Zimbabwe

Jane Nyingi/ AFPE..Picha AFP22 Januari 2009

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai amesema ana imani kuwa viongozi wa jumuia ya Maendeleo kusini mwa Afrika SADC, watatafuta njia za kutatua mgogoro uliopo sasa nchini Zimbabwe.

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe (kushoto) na mkewe Grace(kulia)Picha: AP

Viongozi hao watakutana wiki ijayo nchini Afrika Kusini.Tsvangirai na rais Robert Mugabe walikutana mapema wiki hii mjini Harare lakini walishindwa kufikia mapatano. Mgogoro mkubwa kati ya mahasimu hao unahusu kugawana wizara muhimu, majimbo, pamoja na kuachiliwa huru kwa wapinzani wanaozuiliwa.


Msemaji wa chama cha upinzani MDC,Nelson Chamisa ameeleza kuwa chama chake hakitakubali kujiunga na serikali ya Mugabe ikiwa matakwa ya chama hicho hayatazingatiwa. Baada ya kuvunjika kwa mazungumzo wiki hii kati ya rais Mugabe na Tsvangirai viongozi wa jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC hawakusema lolote licha ya kuitisha mkutano wa dharura utakaofanyika wiki ijayo mjini Pretoria.


Kiongozi huyo wa upinzani alitia saini makubaliano ya kugawana madaraka na rais Mugabe mwezi september mwaka jana, lakini hadi sasa hayajatekelezwa. Mkwamo wa kisiasa nchini Zimbabwe umesababisha matatizo m akubwa kwa wananchi ,upungufu wa chakula na mlipuko wa ugonjwa wa kipundupindu ambao hadi sasa umesababisha vifo vya watu zaidi ya 2,700.

Akizungumza na umati mkubwa wa watu nchini Zimbabwe Tsvangirai alisema na namnukuu "nasema lazima mateso hayo yaishe,kwa ajili yetu sote na taifa zima" mwisho wa nukuu. Aliendelea kusema kwa sasa mfumo mzima wa elimu umevurungika,viwanda vimefungwa na hali ya chakula ni ya kusikitisha hatua ambayo imewafanya Wazimbabwe kuendelea kuteseka.

Mkutano wa wiki ijayo wa viongozi wa SADC utakuwa wa nne kufanywa na viongozi hao,wakizungumzia mzozo wa Zimbabwe tangu uchaguzi mkuu wa mwezi marchi mwaka jana uliokabiliwa na utata. Wakati wa raundi ya kwanza ya uchanguzi mkuu Tsvangirai alimshinda Mugabe hatua iliyosababisha kutokea kwa machafuko. Kisha baadaye Tsvangirai aliamua kujiondoa katika duru ya pili ya uchaguzi huo akidai kushambuliwa kwa wafuasi wake.Hatimaye rais Mugabe alijitangaza mshindi mwezi Juni.

Wadadisi wanasema sera za Rais Mugabe,kama vile hatua ya kuwafukuza nchini Zimbabwe wazungu waliokuwa wakimiliki mashamba makubwa kumeuzorotesha uchumi wa taifa hilo.Hata hivyo kiongoyzi huyo amekuwa akisisitiza hali ni mbaya nchini Zimbabwe kutokana na vikwazo vilivyowekewa serikali yake na mataifa ya magharibi.

Kiongozi mkuu wa majeshi nchini Zimbabwe amesema majeshi yake hayatakubali majeshi ya magharibi kuingia nchini humo katika harakati za kuipindua serikali ya rais Mugabe.Kwa mujibu wa ripoti ya shirika linaloratibu misaada ya kiutu la umoja wa mataifa-OCHA zaidi ya wazimbabwe elfu 48 wanaungua kipindupindu. Ugonjwa huo umeathiri asilimia 88 ya wilaya zote nchini Zimbabwe,tangu kulipuka kwake mwezi Agosti mwaka jana kufutia kuvunjika kwa mfumo wa kupitishia maji taka na pia uhaba wa maji.
















Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW