Viongozi wa SCO wasifia maendeleo ya jumuiya yao
16 Septemba 2022Xi amesema hayo katika mkutano wa kilele wa Jumuiya ya UShirikiano wa Shangai SCO unaofanyika Uzbekistan. Mkutano huo unaohudhuriwa pia na rais wa Urusi Vladimir Putin unatizamwa kuwa ya kukabili ushawishi wa nchi za magharibi duniani.
Mwenyeji wa mkutano huo, rais wa Uzbekistan Shavkat Mirziyoyev ameusifia mkutano huo akisema jukumu la ushirikiano wao kuleta utulivu linaongezeka. Jambo ambalo ni muhimu kiusalama na kiukuaji wa uchumi. Kwenye hotuba yake amesema uchumi wa nchi wanachama wa SCO umeongezeka mara kumi tangu kuanzishwa kwake na inaendelea kukua kwa kasi.
Rais Vladimir Putin ayasifia mahusiano yake na Xi Jinping
"Bila shaka, Mkutano wetu wa ni wa kihistoria. Huu ni mkutano wa ana kwa ana wa marafiki uliosubiriwa kwa muda mrefu baada ya changamoto na ugumu wa janga hili. Hii ni fursa ya mawasiliano ya kibinafsi na kufanya maamuzi ya pamoja ambayo huamua mustakabali wa shirika letu na hatima ya mkoa wa SCO kwa ujumla," amesema Shavkat Mirziyoyev.
Xi ameuambia mkutano huo wa kilele kwamba wanachama wanapaswa kuachana na mitizamo ya 'ushindi wa mmoja ni hasara kwa mwengine', pamoja na siasa za kikanda. Badala yake wazingatie mfumo wa kimataifa na Umoja wa Mataifa katika msingi wake.
Kwa upande wa rais wa Urusi Vladimir Putin, amesifia kile alichokitaja kuwa ushawishi unaokua wa "vituo vipya vya madaraka” vinavyoshirikiana pamoja, na hilo linazidi kuwa bayana. Kulingana na Putin, jumuiya hiyo iko wazi kushirikiana na ulimwengu mzima, huku akizirai jumuiya nyinginezo kuwa na misingi kama yao.
Pendekezo la kuanzishwa mashindano ya jumuiya ya ushirikiano wa SCO
Putin pia aliwasilisha pendekezo kwa viongozi kwenye mkutano huo wa kilele kwamba, wanapaswa kufikiria kuandaa mashindano yao yenyewe ya michezo ya kanda hiyo. Ili kuwezesha hilo amesema wanapaswa kufikiria kuunda chama kitakacholeta pamoja mashirikisho ya michezo ya jumuiya hiyo.
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alitoa wito kwa viongozi wa SCO kushughulikia migogoro ya nishati na chakula, ambayo imechochewa na janga la COVID-19 pamoja na vita nchini Ukraine.
Kulingana na Modi, janga la Covid na mzozo ndani ya Ukraine vimevuruga mambo mengi katika mnyororo wa uzalishaji na ugavi wa bidhaa hizo. Amesema SCO inapaswa kujitahidi
kukuza minyororo imara na ya kutegemewa ya ugavi katika kanda hiyo.
Suala la nishati ni mojawapo ya ajenda ambazo wanachama wa SCO wanatarajiwa kujadili kwenye mkutano huo.
Jumuiya ya ushirikiano wa SCO inajumuisha China, India, Pakistan, Urusi, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan na Uzbekistan. Jumuiya hiyo iliundwa mwa 2001 kama chombo cha kisiasa, kiuchumi na kiusalama kwa taasisi pinzani za Magharibi.
(AFPE, RTRE,)