Viongozi wa Somali wakabiliwa na waranti za kukamatwa
28 Novemba 2024Jubbaland, ambayo inapakana na Kenya na Ethiopia na ni moja ya majimbo matano ya Somalia yenye mamlaka ya ndani, ilimchagua tena rais wa kikanda Ahmed Mohamed Islam Madobe kwa muhula wa tatu katika uchaguzi wa Jumatatu wiki hii.
Hata hivyo, serikali ya kitaifa yenye makao yake mjini Mogadishu, ikiongozwa na Rais Hassan Sheikh Mohamud, iliupinga uchaguzi huo, ikisema ulifanyika bila kuihusisha serikali ya shirikisho.
Naye Mwanasheria mkuu wa Jubbaland alitoa hati ya kukamatwa kwa Rais Mohamud jana usiku, kupitia mahakama ya Kismayo, akimtuhumu kwa uhaini, kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe, na kupanga uasi wa kutumia silaha ili kuvuruga utaratibu wa kikatiba nchini humo.
Hati hiyo haikutoa ushahidi wa tuhuma hizo. Waranti huo ni jibu kwa hati kama hiyo iliyotolewa na mahakama ya kikanda mjini Mogadishu ya kukamatwa Madobe, iliyomtuhumu kwa uhaidi na kufichua taarifa za siri kwa vyombo vya kigeni. Utekelezaji wa hati hizi bado haujulikani, kwa sababu Madobe na Mohamud wote wana vikosi vya kijeshi.