Viongozi wa Somalia washinikizwa na UN kuzungumza
24 Aprili 2021Baraza la usalama la Umoja wa mataifa limepitisha siku ya ijumaa tamko la kuvitaka vyama vyote nchini Somalia kuachana na vurugu na kurudi kwenye meza ya mazungumzo kama njia ya dharura na bila ya kuweka masharti yoyote.
Hatua hiyo ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa imeonesha msisitizo juu ya wasiwasi wake kuhusu mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo ya upembe wa Afrika.
Waraka wa tamko hilo umefafanua kwamba wanachama wa baraza la usalama wameeleza wasiwasi wao mkubwa kuhusu mkwamo wa kisiasa unaoendelea na mivutano miongoni mwa viongozi wa kisiasa nchini Somalia juu ya suala la muundo wa kufanyika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.
Shinikizo la UN
Mnamo mwezi Marchi 31 kufuatia mkutano wa dharura baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa liliiwataka viongozi wa mamlaka ya Somalia kutatua mvutano huo uliopo juu ya mchakato wa uchaguzi.Lakini hilo lilishindikana wakati mamlaka ya kisheria ya rais Mohammed Abdullahi Farmajo yakitiliwa mashaka tangu mwezi Februari baada ya kipindi cha muhula wake madarakani wa miaka minne kumalizika,wakati uchaguzi ukiwa bado haujafanyika.
Hata hivyo bunge la nchi hiyo likaamua kupitisha muswaada wa sheria mwanzoni mwa mwezi huu uliomuongezea rais muda wa kubakia madarakani kwa kipindi cha miaka miwili lakini muswaada huo haukufikishwa katika baraza la Seneti.
Kutokana na hilo vyama vya upinzani vinaikosoa hatua hiyo wanayosema imekwenda kinyume na katiba ya nchi ,lakini pia jumuiya ya kimataifa imeikosoa hatua hiyo.
Kinachotakiwa kueleweka hapa ni kwamba rais wa Somalia na viongozi wakuu wa majimbo matano yenye mamlaka yao ya ndani katika shirikisho la Somalia,walikuwa na makubaliano yaliyofikiwa mwezi Septemba mwaka jana yaliyofungua njia ya kufanyika uchaguzi wa bunge na rais usiokuwa wa moja kwa moja uliotakiwa kufanyika mwishoni mwa 2020 au mwanzoni mwa 2021.
Lakini viongozi hao wakaingia kwenye mvutano wakitafautiana kuhusu namna uchaguzi huo utakavyofanyika na duru kadhaa za mazungumzo ya kujaribu kuuondowa mkwamo huo zikishindikana.
Sheria mpya nchini humo inafungua njia ya kufanyika kwa mara ya kwanza uchaguzi utakaomuhusisha moja kwa moja kila mpiga kura wa nchi hiyo kumchagua kiongozi amtakaye kuanzia mnamo mwaka 2023.
Uchaguzi wa namna hiyo haujawahi kufanyika nchini Somalia tangu mwaka 1969 na wasomali wamekuwa wakipewa ahadi hiyo kwa miaka na hakuna serikali ambayo imefanikiwa kutekeleza hatua hiyo.
Tamko la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa la siku ya ijumaa kadhalika limebaini kwamba mkwamo wa kisiasa nchini humo pia umesababisha kutofuatiliwa kwa masuala muhimu yanayoipa changamoto nchi hiyo kama vile mafuriko,ukame,uvamizi wa nzige,janga la Covid-19 pamoja na vita dhidi ya kundi la wanamgambo wa itikadi kali la al-Shaabab.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Lilian Mtono