1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia: Waziri Mkuu amfukuza mjumbe wa Umoja wa Afrika.

Zainab Aziz Mhariri: Chilumba Rashid
7 Aprili 2022

Viongozi wanaozozana nchini Somalia waliingia kwenye mvutano hapo siku ya Jumatano baada ya Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble kumfukuza mjumbe wa Umoja wa Afrika katika nchi hiyo.

Somalia Präsident Farmajo Premierminister Roble
Picha: Abdirahman Yusuf/AFP/Getty Images

Ofisi ya Waziri Mkuu imemtangaza mjumbe wa Umoja wa Afrika, Francisco Madeira kuwa ni mtu asiyetakikana nchini Somalia kutokana na kujihusisha na vitendo ambavyo haviendani na hadhi yake kama mwakilishi wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika. Mjumbe huyo ameamriwa kuondoka Somalia ndani ya saa 48.

Waziri Mkuu wa Somalia Mohamed Hussein Roble.Picha: Somalian Presidency/AA/picture alliance

Taarifa hiyo iliyochapishwa kwenye Twitter haikufafanua sababu kwa nini Waziri mkuu Roble amechukua uamuzi huo dhidi ya Madeira, mwanadiplomasia kutoka Msumbiji ambaye amekuwa mwakilishi maalum wa Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia tangu 2015.

Lakini ni vigumu kubainisha ni nani hasa ana usemi kuhusu swala la anayeshikilia nafasi ya mwakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Somalia kwani Rais wa nchi hiyo Mohamed Abdullahi Mohamed, maarufu kama Farmajo, ameikosoa hatua ya Waziri Mkuu Roble ambaye ni mpinzani wake na kuieleza kuwa ni kinyume cha sheria.

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed FarmajoPicha: Yasuyoshi Chiba/AFP/Getty Images

Ofisi ya rais pia imeandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba haijawahi kupokea malalamiko ya kuingiliwa kwa mamlaka yake na hivyo haikubali hatua zozote zisizo halali dhidi ya Balozi Francisco Madeira na kwamba Rais Farmajo ameiagiza wizara ya mambo ya nje kuomba msamaha kwa Umoja wa Afrika kutokana na kile alichokiita uamuzi usio halali na wa kizembe kutoka kwa ofisi ya Waziri mkuu ambayo haina idhini ya kuchukua uamuzi kama huo.

Soma Zaidi:UN yaidhinisha kikosi kipya cha AU Somalia

Wiki iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipigia kura kwa kauli moja juu ya kuanzishwa kwa kikosi kipya cha kulinda amani kwa taifa hilo la Pembe ya Afrika, ambapo wanamgambo wa itikadi kali wa Al-Shabaab wamekuwa wakitaka kuipindua serikali ya nchi hiyo iliyo dhaifu kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.

Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kitachukua nafasi ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) vilivyoanzishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa mnamo mwaka 2007.

Wanajeshi wa Kenya wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini Somalia.Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Vikosi hivyo viliwajumuisha wanajeshi kutoka barani Afrika kote, ambao waliendesha operesheni ya kupambana na hatimaye kuwafukuza wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab kutoka kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu mnamo mwaka 2011, hali iliyojenga utulivu kwa serikali na kuimarika kwa mashirika yake pamoja na  kufanyika duru mbili za uchaguzi.

Lakini mzozo mkali wa kuwania madaraka kati ya Farmajo na Roble umezuia juhudi za kuandaa uchaguzi ambao umecheleweshwa kwa muda mrefu baada ya kumalizika muda wa mamlaka ya rais mnamo Februari mwaka jana.

Vyanzo: AFP/RTRE

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW