Rais Kiir kukutana na Machar mjini Addis Ababa
20 Juni 2018Afisa wa cheo cha juu wa vuguvugu la upinzani la ukombozi wa watu wa Sudan, SPLM-IO, Manasseh Zindo, ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba Riek Machar amewasili katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, mapema leo kwa mazungumzo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Ethiopia amethibitisha kuwasili kwa Machar mjini humo, huku mazungumzo kati ya Machar na rais Kiir yakilenga kuondosha tofauti na kuleta maelewano kati yao.
Wachambuzi wanaonya matokeo yanabaki kutokuwa wazi ikizingatiwa mahusiano mabovu yaliyovurugika kabisa kati ya viongozi hao, na bado kuna wasiwasi ikiwa kweli mkutano kati yao utafanyika. Kushiriki kwa rais Kiir katika mazungumzo hayo kumethibitishwa na balozi wa Sudan Kusini nchini Ethiopia, Jamed Pitia Morgan.
Kiir na Machar, ambao walikuwa washirika wakubwa katika vita vya ukombozi vya kupigania uhuru, walikosana vibaya, hatua ambayo ilikuwa na mchango muhimu katika kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini vinavyohatarisha mustakabali wa taifa hilo changa dunaini.
Maelfu ya watu wameuliwa na karibu theluhti moja kati ya watu milioni 12 ya wakazi wamelazimika kuyakimbia makazi yao, na wengi wanakabiliwa na kitisho cha baa la njaa.
Rais Kiir na Machar watakutana kufuatia mualiko wa waziri mkuu mpya wa Ethiopia, Abiy Ahmed, ambaye pia ni mwenyekiti wa Shirika la ushirikiano wa Maendeleo la nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, IGAD, ambalo limejitwika jukumu la kuongoza na kusimamia mazungumzo ya amani ambayo hadi sasa hajazaa matunda.
Kiir na Machar watatakiwa waondoshe tofauti zao
Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za kigeni wa Ethiopia, Meles Alem, amesema waziri mkuu Abiy atawataka viongozi hao kupunguza tofauti zao na kufanya kazi pamoja kwa lengo la kuleta utulivu Sudan Kusini na kuwaondoshea raia mzigo wa mauti na kuepusha kuwaangamiza kabisa watu wa Sudan Kusini.
Machar na Kiir hawajakutana tangu Julai 2016, wakati mapigano makali yaliyozuka katika mji mkuu Juba, yalipoashiria kusambaratika kwa mkataba wa amani ulioafikiwa mwaka 2015 na Machar akatimkua nchini Afrika Kusini. Machafuko mapya yamekuwa yakienea kote nchini, yakiyahusisha makundi kadha wa kadha ya upinzani yaliyojihami na silaha na hivyo kuukwamisha zaidi mchakato wa kutafuta amani.
Licha ya shinikizo, wachambuzi wanasema Kiir hana nia kubwa ya kufanya mapatano na mahasimu wake, huku wanajeshi wake wakiendelea kupata ushindi katika mapigano na wapinzani wakiwa wamegawanyika na kukosa msimamo wa pamoja. Juhudi za kuufufua mkataba amani wa 2015 zilisaidia kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano mwezi Desemba mwaka uliopita, ambayo yalidumu kwa saa chache tu kabla pande zinazopigana kuanza kunyosheana kidole cha lawama kwa kutoyaheshimu.
Mkutano wa leo mjini Addis Ababa unafanyika huku kukiwa na hali ya kukata tamaa katika ngazi ya kimataifa. Mnamo mwezi Mei mwaka huu baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilizipa pande mbili zinazohasimiana Sudan Kusini muda wa mwezi mmoja kuafikia mkataba wa amani au zikabiliwe na vikwazo.
Marekani ilikuwa mshirika na mdhamini mkubwa wa Sudan Kusini wakati ilipojitenga na Sudan, na inabaki kuwa mfadhili mkubwa. Lakini afisa wa cheo cha juu wa Marekani mapema mwezi huu alitishia kuziwekea vikwazo pande zote mbili zinazohusika katika mzozo, baada ya ripoti ya wakfu wa Marekani wa Sentry, kusema kwamba viongozi wa Sudan Kusini wananufaika kutokana na ukiukaji wa haki za binadamu.
Mwandishi: Josephat Charo/afpe
Mhariri: Saumu Yusuf