Viongozi wa Ujerumani na Ufaransa wakutana kukiwapo mivutano
26 Oktoba 2022Rais Macron na Kansela Scholz wameshiriki mazungumzo hayo kwenye hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa katika katika ikulu ya Elsee mjini Paris, ambapo miongoni mwa masuala mengine wamejadili hali ilivyo nchini Ukraine.
Soma zaidi: Mvutano wa Ujerumani na Ufaransa wahujumu hatua za EU
Msemaji wa serikali ya Ufaransa, Olivier Veran amesema ziara ya Kansela Scholz inaonyesha uwezo wa nchi mbili, Ufaransa na Ujerumani kuzikabili tofauti baina yao pale maslahi ya nchi moja yanapogongana na ya nchi nyingine.
''Ziara ya Kansela wa Ujerumani kukutana na rais wa Ufaransa ni ushahidi wa urafiki ulio hai kabisa, na dhamira yetu ya kusonga mbele pamoja, na wakati mwingine kuvivuka vizuizi,'' amesema Veran na kuongeza kuwa nguvu ya uhusiano baina ya Ufaransa na Ujerumani iko katika kukubaliana kila wakati kuuinua Umoja wa Ulaya.
Kikao cha pamoja cha mawaziri chaahirishwa
Mipango ya awali ilihusisha pia kikao cha pamoja cha mabaraza ya mawaziri ya Ufaransa na Ujerumani, lakini hicho kiliahirishwa hadi Januari. Serikali za nchi hizo zimesema yapo mambo yanayojadiliwa kwanza kabla ya kupata muafaka juu ya masuala yanayohusu pande mbili.
Soma zaidi: Viongozi wa Ujerumani, Ufaransa na Italia waizuru Ukraine
Tofauti kati ya Ujerumani na Ufaransa sio kitu kipya. Nchi hizo zenye uchumi mkubwa zaidi katika Umoja wa Ulaya na zinazotazamwa kama injini ya umoja huo, zimezoea kuwa na mitazamo inayokinzana juu ya usalama, nishati na masuala mengine.
Akizungumza mjini Brussels wiki iliyopita, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alisema lengo lake mara zote limekuwa kuimarisha umoja wa Ulaya na mahusiano mema na Ujerumani, na kuongeza kuwa kujitenga kando kwa Ujerumani hakuna tija kwa nchi hiyo wala kwa Ulaya kwa ujumla.
Scholz asema anawasiliana mara kwa mara na Macron
Alipoulizwa Ijumaa iliyopita ikiwa kuna mvutano baina ya nchi yake na Ufaransa, Kansela Scholz alijibu tu kuwa uhusiano baina ya nchi hiyo ni imara, na kuongeza kuwa huwa anafanya mazungumzo ya mara kwa mara na Rais Emmanuel Macron.
Soma zaidi: Putin awaonya Scholz na Macron dhidi ya kuipa silaha Ukraine
Vikao vya pamoja vya mawaziri wa Ufaransa na Ujerumani kwa kawaida hufanyika angalau mara moja kila mwaka, na cha mwisho kilifanyika kwa njia ya vidio mwezi Mei mwaka jana.
Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Hebestreit alisema kuwa bado yapo mambo ambayo yanauzonga kila upande, na hakuna uhakika kama nchi hizo mbili zina mitazamo sawia juu ya baadhi ya mambo ya kimsingi.
Vyanzo: ape, dpae