1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ujerumani, Ufaransa na Italia waizuru Ukraine

Daniel Gakuba
16 Juni 2022

Viongozi wa nchi tatu zinazoongoza kiuchumi barani Ulaya, Ujerumani, Ufaransa na Italia, wamewasili katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev, katika ziara inayonuiya kuonyesha mshikamano wa Ulaya na Ukraine.

Mario Draghi, Emmanuel Macron und Olaf Scholz im Zug nach Kiew
Kuanzia kushoto: Waziri mkuu wa Italia Mario Draghi, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakiwa njiani kuelekea KievPicha: Ludovic Marin/AFP

Taarifa ya Ikulu ya Ufaransa imesema viongozi hao watatu; Kansela Olaf Scholz, Rais Emmanuel Macron na Waziri Mkuu Mario Draghi wamesafiri pamoja kwa treni kutoka nchini Poland hadi Kiev, na kwamba wameungana na rais wa Romania Klaus Iohannis aliyewasili baadaye. Mara baada ya kuwasili Kiev, Rais Macron amesema ziara yao ni hatua muhimu.

Soma zaidi: Putin awaonya Scholz na Macron dhidi ya kuipa silaha Ukraine

''Tuko hapa na tuko makini, na tutazungumza na rais Zelenskiy na kutembelea maeneo ambako mauaji yalifanyika, nadhani ni wakati muhimu. Kwa Waukraine tunao ujumbe wa mshikamano na uungaji mkono,'' amesema Macron na kuongeza kuwa watazungumza juu ya yanayojiri kwa sasa na juu ya mustakabali wa nchi, kwa sababu ''tunajua wiki zijazo zitakuwa ngumu sana.''

Kitongoji cha Irpin walichokitembelea Scholz, Macron na Draghi kilishuhudia mapigano makali wakati kikikaliwa na wanajeshi wa UrusiPicha: Carol Guzy/Zumapress/picture alliance

Wafika Irpin, Macron asema uhalifu wa kivita ulifanyika

Eneo walilolizuru viongozi hao lililoshuhudia mauaji makubwa ni kitongoji cha Irpin cha mji mkuu Kiev, ambako kulipatikana miili ya raia 300 baada ya wanajeshi wa Urusi waliokuwa wakikikalia kuondoka mwishoni mwa mwezi Machi. Walifika huko wakisindikizwa na Oleksiy Chernyshov, mjumbe wa rais Volodymyr Zelenskiy kuhusu mchakato wa Ukraine kutaka kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Katika kitongoji hicho, Rais Emmanuel Macron amesema inadhihirika kuwa uhalifu wa kivita ulifanyika.

Soma zaidi: Zelensky: Vikosi vya Urusi vinaendelea kuishambulia Kiev  

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amenukuliwa na shirika la habari la Ujerumani, dpa akisema yeye na viongozi wenzake wanaazimia kuonyesha utashi wao wa kuendelea kuisaidia Ukraine kifedha na kwa mahitaji ya kibinadamu, na pia kuipatia silaha, kwa muda wote ambao Ukraine itauhitaji msaada huo kupigania uhuru wake.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amekuwa akiomba jeshi la nchi yake lipatiwe silaha za kupambana na UrusiPicha: Ukrainian Presidential Press Office via AP/picture alliance

Scholz pia amesema vikwazo dhidi ya Urusi ni muhimu, kwa sababu vinaweza kuishinikiza Urusi kuondoa wanajeshi wake kutoka Ukraine.

Ishara muhimu ya mshikamano

Viongozi hao wa Ujerumani, Ufaransa na Italia wamesafiri usiku katika treni iliyotolewa na Ukraine, na wakati wa safari yao wamekuwa na mazungumzo marefu ya kujaribu kuwianisha misimamo yao kabla ya kukutana na rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy.

Soma zaidi: Marais wa Ujerumani na Ukraine wasuluhisha mzozo wao

Ziara yao ni ishara muhimu, kwa sababu nchi zao zimekuwa zikikosolewa kutofanya vya kutosha kuipa Ukraine silaha ambazo imekuwa ikiziomba, na pia kwa msimamo wao wa kuendelea kuzungumza na rais wa Urusi, Vladimir Putin. Waukraine wengi pia wanaitazama ziara ya viongozi hao kwa matumaini kuwa inaweza kufungua njia ya enzi mpya ya kuipatia nchi yao zana za kijeshi inaziozihitaji kukabiliana na uvamizi wa Urusi.

rtre, afpe

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW