1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ujerumani walaani jaribio la kuvamia bunge

31 Agosti 2020

Viongozi wa Ujerumani wamelaani jaribio la waandamanaji kuvamia Jengo la bunge wakati wa maandamano dhidi ya vikwazo vya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona na kusema hatua hiyo haikubaliki

Neue Wohlfahrtsmarken
Picha: picture-alliance/dpa/W. Kumm

Baadhi ya waandamanaji hao siku ya Jumamosi walibeba bendera ya zamaninya Ujerumani iliyotumika hadi mwishoni mwa vita vya kwanza vya dunia. Katika ujumbe kupitia mtandao wa Instagram, rais wa Ujerumani Frank -Walter Steinmeier amesema kuwa bendera hiyo ni udhalilishaji wa mrengo mkali wa kulia mbele ya bunge la Ujerumani na ni mashambulizi yasiokubalika katika demokrasia ya nchi hiyo. Aliongeza kwamba hawatakubali mienendo hiyo.

Steinmeier alisema kuwa watu wana haki ya kuelezea ghadhabu yao kuhusu vikwazo hivyo vya kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya corona na kuvitilia shaka ikiwa ni pamoja na kufanya maandamano lakini akaongeza kuwa uvumilivu wake unafikia mwisho wakati waandamanaji wanaruhusu kutumiwa na maadui wa demokrasia na wachochezi wa kisiasa.

Waandamanaji nje ya jengo la bunge mjini BerlinPicha: Reuters/C. Mang

Wakati huo huo naibu Chansela wa Ujerumani Olaf Scolz amesema kuwa haikubaliki na haiwezi kuvumiliwa kwamba baadhi ya watu wanasimama mbele ya jengo la bunge la Reishstag, alama muhimu zaidi ya demokrasia ya nchi hiyo ambalo ni bunge wakiwa na alama za siku mbaya zilizopita wakiwa na bendera ambazo hazina maana katika demokrasia yetu ya kisasa . Nawashukuru sana maafisa wa polisi walioonesha kujitolea kwao na lazima tufanye kila tuwezalo kuhakikisha matukio kama hayo hayatumiwi tena mbele ya jengo la bunge.

Katika ujumbe kupitia mtandao wa twitter, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema kuwa bendera ya zamani ya Ujerumani mbele ya jengo la bunge ni fedheha. Wakati huo huo, Spika wa bunge la Ujerumani Wolfgang Schaeuble amekashifu vikali matukio hayo ya Jumamosi na kusema kuwa inawahusu watu wote wakati kundi la wachache la mrengo mkali wa kulia linajaribu kuvamia kiti cha uwakilishi wa watu.

Polisi inasema kuwa takriban watu elfu 38 hii ikiwa idadi mara mbili zaidi iliyotarajiwa, walikusanyika mjini Berlin siku ya Jumamosi kuandamana dhidi ya vikwazo hivyo ambavyo ni kuvaa barakoa na kuacha mwanya kati ya mtu na mwingine.

Siku ya Alhamisi, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na viongozi wengine 16 wa majimbo ya shirikisho la Ujerumani  waliidhinisha vikwazo vikali vya kukabiliana na kuenea kwa janga hilo vinavyojumuisha faini ya dola 59 kwa wale watakaopatikana hawajavaa barakoa ambazo ni lazima.