1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya kudumisha makubaliano ya nyuklia

Yusra Buwayhid
17 Mei 2018

Wakiwa katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya, viongozi wamekubaliana kuendeleza makubaliano ya nyuklia na Iran pamoja na kudumisha ushirikiano wa kiuchumi ulioanza kufufuka tena, baada ya Marekani kujiondoa.

Bulgarien EU-Balkan-Gipfel in Sofia | Donald Tusk
Picha: picture alliance/AP Photo/V. Mayo

Viongozi hao wa nchi wanachama 28 hawakufanya maamuzi ya haraka katika mkutano wao ulioanza Jumatano, ambao ni wa kwanza juu ya suala hilo tokea Trump kujiondoa mapema mwezi huu.

Kujiondoa kwa Trump kulifuatiwa na amri yake ya kutaka kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Iran pamoja na kampuni zozote za Ulaya zitakazofanya biashara nayo. Shirika la nishati la Kifaransa la Total, Jumatano limeungana na mashirika mengine ya barani Ulaya katika kutahadharisha kwamba huenda wakaondoa mradi wao wa gesi wenye thamani ya mabilioni ya dola nchini Iran, wakiwa na wasiwasi iwapo viongozi wa nchi za Ulaya wanaojaribu kuyanusuru makubaliano ya nyuklia ya Iran wana uwezo wa kuilinda biashara yao na Iran.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk amemkosoa vikali Rais wa Marekani na kusema Ulaya imshukuru Rais Trump kwa kuwagutua kwamba walikuwa wakijidanganya, na kwamba hatua ya Trump imewafanya watambue lazima wajisaidie wenyewe bila ya Marekani.

"Bara la Ulaya ama litakuwa eneo lenye ushawishi au kibaraka. Ulaya lazima ishikamane kiuchumi, kisiasa na kijeshi kuliko ilivyokuwa zamani. Kwa ufupi ama tushikamane pamoja au hatutakuwa chochote," amesema Donald Tusk.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakiwa mjini Sofia, Bulgaria.Picha: Reuters/S. Nenov

Mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Junker, aliwasilisha suluhisho kadhaa za kuweza kulinda uwekezaji wa Ulaya nchini Iran na pole pole kufufua ushirikiano wa kiuchumi, ambao mataifa mengi ya Ulaya wanatarajia kunufaika. Miongoni mwa mapendekezo yake ni pamoja na kuiruhusu Benki ya Uwekezaji ya Ulaya kuwekeza nchini Iran.

Duru moja ya Umoja wa Ulaya imesema viongozi hao wamekubaliana kuanza kazi ya kuzilinda kampuni za Ulaya zitakazo athirika na uamuzi wa Trump.

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza, Ujerumani na Ufaransa wamekutana na mwenzao wa Iran Mohammad Javad Zarif mjini Brussels, Jumanne iliyopita na kuwapa kazi wataalamu wao ya kutayarisha hatua zitakazoweza kutumika na kuziwasilisha katika mkutano wa manaibu wao mawaziri mjini Vienna wiki ijayo.

Nchi hizo tatu za Ulaya ni miongoni mwa nyengine tano zilizosaini makubaliano hayo mnamo mwaka 2015 ikiwamo na Marekani kabla ya kujiondoa.

Trump ameyakosoa makubaliano hayo kwa kusema kwamba hayatoizuia Iran kuendeleza mpango wake wa silaha za kinyuklia, na kwamba makubaliano hayo hayajagusia mpango wa Iran wa makombora  na kujiingiza kwake katika migogoro ya Mashariki ya Kati.

Na Iran nayo imesema itaanza kuzalisha tena madini ya Uranium kama haitofaidika kiuchumi kwa kubaki katika makubaliano hayo, ambayo yaliiondolea vikwazo vya kimataifa Jamhuri hiyo ya Kiislam ili isimamishe shughuli zake ya kinyuklia.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/Reuters/afp

Mhariri: Grace Patricia Kabogo