1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

Mkutano wa kuisaidia Syria wafanyika Saudi Arabia

12 Januari 2025

Wanadiplomasia wakuu kutoka eneo la Mashariki ya Kati na barani Ulaya, wamewasili siku ya Jumapili katika mji mkuu wa Saudi Arabia wa Riyadh, kwa mazungumzo ya kuisaidia Syria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Asaad al-Shaibani (kushoto) akiwasili Riyadh
Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Asaad al-Shaibani (kushoto) akipokelewa na viongozi wa Saudi Arabia mjini Riyadh.Picha: Syrian Foreign Ministry Telegram Channel/AFP

Mataifa yenye nguvu duniani yanashinikiza kuwepo kwa hali ya utulivu baada ya kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad. Mazungumzo hayo yatawakutanisha maafisa wa Kiarabu, wawakilishi wa Uturuki, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa.

Saudi Arabia, nchi yenye uchumi mkubwa zaidi katika ukanda wa Mashariki ya Kati, inataka kuongeza ushawishi wake nchini Syria baada ya muungano wa waasi ukiongozwa na kundi la itikadi kali la Hayat Tahrir al-Sham (HTS) kumuangusha Assad mwezi uliopita.

Kiongozi mpya wa Syria Ahmed al-Sharaa, ambaye aliongoza kundi hilo kumwangusha Assad, anashinikiza taifa hilo kuondolewa vikwazo. Utawala wake unawakilishwa katika mazungumzo ya Riyadh na Waziri wa Mambo ya Nje Asaad al-Shaibani.

Soma pia: Wanadiplomasia wa nchi za Kiarabu na Ulaya wakutana Saudia kuisaidia Syria

Mataifa yenye ushawishi ya Magharibi, ikiwa ni pamoja na Marekani na Umoja wa Ulaya, yaliuwekea vikwazo utawala wa Assad kutokana na ukandamizaji wake wa kikatili dhidi ya maandamano ya kuipinga serikali yake mwaka 2011, ambayo yalizusha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Vita hivyo vilivyodumu kwa miaka 13 vimesababisha vifo vya zaidi ya Wasyria nusu milioni, miundombinu iliharibiwa na watu wakisukumwa kwenye umaskini, huku mamilioni ya wengine wakiyakimbia makazi yao, huku baadhi wakielekea barani Ulaya.

EU kuamua Januari kuhusu kuilegezea vikwazo Syria

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja KallasPicha: Alexandros Michailidise/European Union

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas amesema mawaziri wa mambo ya nje wa umoja huo watakutana mwishoni mwa mwezi Januari ili kujadili kuhusu kuilegezea vikwazo Syria.

Kallas ameyasema hayo Jumapili mjini Riyadh kabla ya mkutano wa viongozi wakuu wa Mashariki ya Kati, wanadiplomasia wa Magharibi pamoja na waziri mpya wa mambo ya nje wa Syria na kusisitiza kuwa mawaziri hao wa EU watakutana mjini Brussels, Ubelgiji mnamo Januari 27 katika juhudi za kuamua jinsi jumuiya hiyo ya mataifa 27 italegeza vikwazo dhidi ya serikali ya sasa ya  Syria.

Uamuzi wowote wa Ulaya wa kulegeza vikwazo utaambatana na masharti kuhusu mfumo mpya wa utawala wa Syria katika suala la kuyajumuisha "makundi tofauti" pamoja na wanawake na kuepusha "itikadi kali", alisema Kallas bila hata hivyo kutoa ufafanuzi zaidi.

Kallas aliendelea: "Ikiwa tutashuhudia maendeleo yanayoelekea katika mwelekeo sahihi, sisi tuko tayari kufikia hatua zinazofuata...Tukiona kwamba hayaendi katika mwelekeo sahihi, basi tunaweza pia kurejea kwenye vikwazo hivi."

Ujerumani: Baadhi ya vikwazo kuendelea kutekelezwa

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema siku ya Jumapili kwamba vikwazo dhidi ya maafisa wa Syria waliohusika na uhalifu wa kivita ni lazima viendelee kutekelezwa lakini akatoa wito wa kuwepo "hatua za busara" zitakazowezesha kutoa unafuu kwa wakazi wa Syria baada ya kupinduliwa kwa Rais Bashar Assad mwezi uliopita.

Baerbock alizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili Saudi Arabia kuhudhuria mkutano unaojadili kuhusu mustakabali wa Syria.  Ujerumani ni moja kati ya nchi kadhaa za Ulaya zilizoiwekea vikwazo serikali ya Assad kutokana na ukandamizaji wake wa kikatili dhidi ya wapinzani.

Kwa sasa Wasyria wanahitaji kushuhudia faida zitokanazo na utawala huu wa mpito. Ujerumani ilitangaza nyongeza ya dola milioni 51.2 katika msaada wa  chakula, malazi ya dharura na matibabu ikizingatia hali mbaya inayowakabili mamilioni ya Wasyria waliokimbia makazi yao kutokana na vita.

Marekani yalegeza vikwazo kwa viongozi wa Syria

Ahmad al-Sharaa, kiongozi wa sasa wa SyriaPicha: Khalil Ashawi/REUTERS

Wiki iliyopita, Marekani ililegeza baadhi ya vikwazo vyake kwa Syria, na kuidhinisha kwa muda wa miezi sita kufanya miamala kadhaa na serikali ya Syria, ikiwa ni pamoja na baadhi ya mauzo ya nishati.

Soma pia: Assad ameondoka: Je, Syria bado inastahili kuwekewa vikwazo?

Marekani iliondoa pia fidia ya dola milioni 10 ambayo ilikuwa imetolewa kwa yoyote ambaye angeliwezesha kukamatwa kwa Ahmad al-Sharaa, kiongozi wa waasi wa Syria ambaye zamani alijulikana kama Abu Mohammed al-Golani, ambaye vikosi vyake vya HTS viliongoza muungano uliofanikiwa kumuondoa Assad madarakani.

Al-Sharaa aliwahi kuwa mwanamgambo mkuu wa al-Qaida  lakini kwa miaka kadhaa sasa alijitenga na kundi hilo na kujikita kwenye harakati za kuijenga  Syria iliyo jumuishi na inayoheshimu haki za watu wote.

(Vyanzo: DPA, AP, Reuters, AFP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW