1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya wahimiza umuhimu wa kujisimamia kiulinzi

8 Novemba 2024

Viongozi wa mataifa yanayokaribia 50 ya Ulaya wametoa mwito wa kuwekwa mkakati madhubuti wa ulinzi wa bara hilo usioitegemea moja kwa moja Marekani.

Budapest | Mkutano wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya mjini Budapest, Hungary.
Viongozi wa mataifa ya Ulaya wakihudhuria mkutano wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya mjini Budapest, Hungary. Picha: Filippo Attili/ZUMA Press/IMAGO

Wito huo umetolewa katika wakati hali ya wasiwasi imerejea kufuatia ushindi unaomrejesha Donald Trump madarakani.

Kwenye mkutano wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya uliofanyika jana mjini Budapest nchini Hungary, viongozi hao waliliweka mezani suala la ulinzi na usalama wa Ulaya na kutathimini dhima ya mataifa ya bara hilo pasipo kuitegemea Washington.

Mwenyeji wa mkutano huo Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban, amesena viongozi waliokutana wameafikiana kuwa Ulaya inafaa ichukue jukumu kubwa zaidi la ulinzi na usalama wake badala ya kuisubiri Marekani.

Ushindi wa Trump katika uchaguzi wa Marekani mapema wiki hii umezusha mashaka hasa ikizingatiwa alitumbukia kwenye mivutano na washirika wake alipokuwa madarakani miaka minne iliyopita.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, amewaambia wenzake walioshiriki mkutano wa Budapest kwamba Trump amechaguliwa na Wamarekani na atalinda maslahi ya nchi yake na kuwarai viongozi wa Ulaya kutafakari iwapo wako tayari kuyalinda mataifa yao.