Ulaya kufanya mazungumzo na Bosnia juu ya kujiunga na EU
22 Machi 2024Mazungumzo hayo yataanza mara baada ya nchi hiyo ya ukanda wa Balkan itakapopitisha mageuzi muhimu katika idara ya mahakama na mfumo wa uchaguzi.
Rais wa baraza la Ulaya Charles Michel ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa X, akiipongeza Bosnia na kueleleza kuwa nchi hiyo inakaribishwa kujiunga na familia ya Umoja wa Ulaya.
Soma pia: Uholanzi yaiomba radhi Srebrenica kwa mauaji
Bosnia imepewa hadhi ya kuwa mgombea wa nafasi ya uanachama wa Umoja wa Ulaya tangu mwaka 2022 japo ilihitajika kufanya msururu wa mageuzi kabla ya mchakato huo kupelekwa katika hatua nyengine.
Wiki iliyopita, Umoja wa Ulaya ilisema kuwa nchi hiyo imepiga hatua japo haijafanya mageuzi katika idara ya mahakama na mfumo wa uchaguzi.
Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umeuchochea msukumo wa Umoja wa Ulaya kutanua kuelekea Ulaya Mashariki na Kati. Mnamo mwezi Disemba, nchi wanachama zikikubaliana kuanza mazungumzo ya Ukraine na Moldova kujiunga na Umoja huo.