Viongozi wa Ulaya wakutana kujadili njia za kukabiliana na mgogoro wa fedha
4 Oktoba 2008Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa ambaye nchi yake hivi sasa inashikilia urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya atakuwa mwenyeji wa mkutano huo utakohudhuriwa na viongozi wa Ujerumani,Uingereza na Italia.Ujerumani imelikataa pendekezo lililowasilishwa na Ufaransa la kuwepo kwa mfuko wa euro bilioni 300 kuzipa nguvu benki zenye matatizo.
Ujerumani na Uingereza nchi zote mbili zimekuwa zikikataa kutowa fedha za walipa kodi kwa mfuko huo utakaosimamiwa na Umoja wa Ulaya.Badala yake zimependekeza hatua zichukuliwe kwa kutegemeana na kesi kuokowa taasisi za kifedha.
Viongozi wa Ulaya wanatumai kuwa na msimamo wa pamoja juu ya namna ya kukabiliana na kimbunga hicho cha fedha kilichozushwa na mgogoro wa mabenki ya Marekani kabla ya mkutano wa mawaziri wa fedha wa Kundi la Mataifa Manane yenye maendeleo makubwa ya viwanda duniani utaofanyika mjini Washington wiki ijayo.