Viongozi wa Ulaya wapanda jukwaani Davos
20 Januari 2026
Von der Leyen alikuwa akizungumza Davos nchini Uswisi kulikofunguliwa rasmi Jukwaa la Kiuchumi la Dunia, ambapo ameutilia shaka uaminifu wa Trump akisema, mwaka jana alikubali kutoziwekea ushuru zaidi nchi za Umoja wa Ulaya.
Wakati huo huo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema ulimwengu unapitia kipindi ambacho sheria za kimataifa zinapuuzwa na sheria zinazoonekana kuwa zenye umuhimu ni zile za wenye nguvu tu.
Akiwa Davos, Macron ameilaani hatua ya Marekani kutaka kuidhoofisha Ulaya kupitia makubaliano ya kibiashara ambayo yanakiuka maslahi yake ya uuzaji bidhaa nje na kulitaka bara hilo likubaliane kikamilifu na matakwa yake.
Aidha, Macron amesema hakuna mkutano wa kundi la mataifa saba yaliyoendelea kiuchumi duniani ya G7, uliopangiwa kufanyika siku ya Alhamisi.