Viongozi wa ulimwengu waanza kuwasili London kumuaga Malkia
17 Septemba 2022Leo Jumamosi wana mfalme William na Harry wakitarajiwa kuwaongoza wajukuu zake Malkia kwenye shughuli ya kutoa heshima zao za mwisho kwenye jeneza lake. Siku ya Ijumaa Mfalme wa Uingereza Charles wa tatu na ndugu zake walisimama karibu na jeneza la mama yao marehemu Malkia Elizabeth wa pili kutoa heshima zao huku maelfu ya waombolezaji wakiwa kwenye foleni ndefu wakisubiri nao kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi wao.
Walielezwa kwamba huenda wangelisubiri kwenye foleni hiyo kwa saa 24 kabla ya kupata fursa ya kumuaga Malkia Elizabeth wa pili. Mistari hiyo ni mirefu mno kando ya Mto Thames tangu siku ya Jumatano wakati jeneza la malkia Elizabeth wa pili lilipoletwa kwenye jumba la bunge la Uingereza, Westminster.
Mfalme Charles wa tatu, Princess Anne, Prince Andrew na prince Edward, wakiwa wamevalia sare za kijeshi, walisimama kimya na kuinamisha vichwa vyao kwa dakika 15 katika Ukumbi wa kihistoria wa Westminster ambapo jeneza la marehemu malkia wa Uingereza limewekwa hapo tangu siku ya Jumatano kwa ajili ya kuagwa kabla ya kuzikwa hapo siku ya Jumatatu tarehe 19.
Kifo cha malkia huyo wa Uingereza kilitokea mnamo Septemba 8 akiwa na umri wa miaka 96, baada ya kutawala kwa miaka 70 kwenye kiti cha enzi.
Mrithi wa malkia, Mfalme Charles III, atakutana Jumamosi na mawaziri wakuu wa mataifa ya Jumuiya ya Madola ambayo ni makoloni 14 ya zamani ya Uingereza. Australia, New Zealand na Kanada, zimemtangaza rasmi kuwa Mfalme Charles wa tatu kuwa ni mtawala wao mpya.
Umma una hadi Jumatatu asubuhi kulitazama jeneza la Malkia Elizabeth wa pili kabla ya kufanyika mazishi ya kwanza ya kiserikali nchini Uingereza kwa karibu miongo sita.
Hafla hiyo ya kuuga mwili wa Malkia itafanyika katika kanisa la Westminster Abbey na inatarajiwa kutazamwakwenye runinga na mamilioni ya watu duniani kote. Wageni zaidi ya 2,000, wamealikwa isipokuwa viongozi kutoka nchi zinazozozana na Uingereza kama Urusi, Belarus na Afghanistan hawakualikwa. Mazishi ya faragha yatafuata katika kasri ya Windsor baada ya ibada.
Chanzo:AFP