Viongozi wa EU kujadili uhamiaji
6 Oktoba 2023Katika mkutano unaofanyika Granada Uhispania, viongozi hao wataangazia suala la uhamiaji wakati mataifa ya Umoja wa Ulaya yakishuhudia ongezeko la kuwasili kwa wahamiaji. Licha ya kupigwa kwa hatua katika maajadiliano ya kutafuta mabadiliko, uhamiaji umesalia kuwa mada inayozigawa nchi wanachama.
Waziri Mkuu wa Italia Georgio Meloni anatarajiwa kufanya mazungumzo na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz katika mkutano wa pembeni baada ya Meloni kuonesha kushangazwa kwake na usaidizi wa kifedha kwa shirika la kiraia la kusaidia kuwaokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediterania.
Akizungumzia suala la uhamiaji, Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban amesema kuwa makubaliano kuhusu suala la uhamiaji katika mkutano wa leo wa viongozi wa Umoja wa Ulaya hayawezi kupatikana.
Orban ametoa kauli hiyo baada ya nchi yake kushindwa katika kura iliyopigwa mapema wiki hii kuhusu suala linalohusiana na uhamiaji.
Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umeifanya Ulaya ipunguze utegemezi.
Katika hatua nyingine, Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel amesema kuwa, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo mwezi Februari mwaka uliopita, umeifanya Ulaya ipinguze utegemezi wake wa nishati na kujenga msingi imara zaidi wa uchumi.
Amesema mkutano huo wa Granada ni muafaka katika kutazama mbele ili kupata mkakati utakaohakikisha uthabiti wa Umoja wa Ulaya na ushindani katika mazingira magumu ya kisiasa na kijiografia.
Majadiliano ya viongozi wa Umoja wa Ulaya yanayofanyika leo yatasaidia kuendesha mazungumzo kuhusu mapendekezo ya umoja huo yatakayoweza kuleta udhibiti mkali zaidi wa usafirishaji wa bidhaa na utolewaji wa teknolojia, hasa zile zinazoweza kutumika kijeshi.
Hadi kufikia mwisho wa mwaka, tume ya umoja huo inapanga kufanya kazi na mataifa 27 wanachama ili kutathmini ikiwa kuna hatari yoyote inayohusiana na akili bandia, teknolojia ya fizikia na baiolojia.