Hali ya maisha ya kawaida yabadilika Ulaya kufuatia Corona
16 Machi 2020Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imesema hatua ya kufunga mipaka sio njia bora ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona katika umoja huo. Kauli hiyo imetolewa leo wakati nchi mbali mbali za bara hilo ikiwemo Ujerumani zikichukua hatua hiyo miongoni mwa nyingine.
Tukianzia hapa barani Ulaya viongozi wanajiandaa kufanya mkutano wa kilele wa dharura kesho Jumanne kwa njia ya vidio kuhusiana na hali ilivyo mpaka kufikia sasa kuhusu ugonjwa huo wa virusi vya Corona.
Rais wa baraza la Ulaya Charles Michel akitoa taarifa amesema suala muhimu linaloangaziwa na umoja huu kwa sasa ni jinsi ya kuzuia kuenea kwa maambukizi, kusambaza vifaa tiba zaidi pamoja na kuimarisha utafiti na kuzuia athari za kiuchumi zinazoweza kusababishwa na ugonjwa huo.
Viongozi hao wa Ulaya wanakutana wakati kila nchi ikiwa imezidi kuchukua hatua ya kujaribu kukabiliana na kusambaa kwa ugonjwa huo ikiwemo kufunga mipaka, shule, mikahawa na kuweka sheria kali katika masuala mengine ya shughuli za kijamii. Ugiriki mojawapo ya nchi zilizoko ndani ya Umoja wa Ulaya imethibitisha visa 331 vya watu walioambukizwa virusi vya Corona na watu wanne wameshakufa kutokana na virusi hivyo.
Nchi hiyo imefikia uamuzi wa kufunga maduka yote ya reja reja kuanzia siku ya Jumatano. Lakini pia mji mkuu Athens umepiga marufuku meli zote za usafiri wa abiria kutoka Italia kutia nanga kwenye bandari zake.
Nchini Uswizi nako hatua mbali mbali zimechukuliwa ikiwemo kufutiliwa mbali kwa vikao vya bunge la taifa. Nchi hiyo imeripoti visa vipya jumla ya 840 kufikia jana Jumapili na kuifanya idadi hiyo ya wenye virusi vya Corona nchini humo kufikia watu 2,200 sawa na idadi iliyorekodiwa katika nchi jirani yake ya Liechtenstein.
Idadi hiyo imetajwa kuwa ni zaidi ya asilimia 50 kwa siku moja hali ambayo inaonesha kwamba maambukizi ya ugonjwa huo yanaongezeka kwa kasi kubwa. Kadhalika barani Ulaya mashirika mengi makubwa ya ndege yametangaza leo Jumatatu yatapunguza safari zao kwa hadi asilimia 90 kufuatia kushuka kwa idadi ya wateja.
Mashirika ya Air France na KLM yamesema yamechukua hatua hiyo kutokana na sheria za kuzuiwa wasafiri wengi kutoka Ufaransa, Uholanzi na nchi nyingine nyingi za Ulaya. Katika eneo la Mashariki ya Kati Iran imesema virusi vya Corona vimeuwa watu wengine 129 na kuifanya idadi ya waliokufa kwa ugonjwa huo nchini humo kufikia 853 huku waliothibitika kuambukizwa wakifikia 14,991. Iran inapambana kujaribu kuzuia kusambaa kwa mripuko huo ingawa idadi hiyo ya waliokufa leo ndio idadi kubwa zaidi tangu lilipozuka janga hilo.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Josephat Charo