1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wailalamikia Urusi

30 Novemba 2013

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameishutumu Urusi Ijumaa(29.11.2013)kwa kuingilia masuala ya ndani ya Ukraine baada yanchi hiyo kutupilia mbali makubaliano na Umoja wa Ulaya yenye lengo la kuivuta karibu na Umoja wa huo.

Germany's Chancellor Angela Merkel is welcomed by Lithuanian President Dalia Grybauskaite, European Council President Herman van Rompuy and European Commission President Jose Manuel Barroso (L-R) at the EU Eastern Partnership summit in Vilnius November 29, 2013. REUTERS/Ints Kalnins (LITHUANIA - Tags: POLITICS BUSINESS)
Viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wa VilniusPicha: Reuters

Hatua hiyo ya Ukraine ya kubeza imeonyesha kuzuka kwa mvutano unaoendelea baina ya Umoja wa Ulaya na Urusi kuhusiana na mataifa yaliyokuwa zamani katika iliyokuwa umoja wa kisovieti mashariki mwa Ulaya.

Jose Barroso mjini VilniusPicha: Janek Skarzynski/AFP/Getty Images

Cha muhimu ni uhuru kamili

"Nyakati za kuwa na uhuru wa kiwango fulani tu zimepitwa na wakati katika bara la Ulaya," rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso amesema mwishoni mwa mkutano huo.

"Hatuwezi kukubali , kuwa na aina fulani ya veto kwa nchi ya tatu. Hii ni kinyume na misingi yote ya sheria za kimataifa," ameongeza.

Mkutano huo wa siku mbili katika mji mkuu wa Lithuania , Vilnius katika eneo la mashariki ya Umoja wa Ulaya ulikuwa uwe ni mwanzo wa msukumo wa miaka mitano wa kuimarisha mahusiano baina ya kundi hilo la mataifa na Belarus, Ukraine, Moldova, Georgia , Armenia na Azerbaijan.

Rais wa Ukraine Viktor JanukovichPicha: Janek Skarzynski/AFP/Getty Images

Lakini rais wa Ukraine Viktor Yanukovich aliziba masikio dhidi ya rai kutoka kwa viongozi wa kundi hilo lenye mataifa wanachama 28 kukubali mkataba huo wenye mambo mengi ya kibiashara na kisiasa, akisema mbinyo wa kiuchumi kutoka Moscow, nchi ambayo inapingana na makubaliano hayo, unaathiri uchumi wa nchi yake.

Maandamano yaendelea

Maelfu ya waandamanaji wanaopendelea makubaliano hayo na mataifa ya magharibi waliingia mitaani katika miji mbali mbali ya Ukraine wakipinga msimamo wa kiongozi wao na kutoa wito ajiuzulu.

Wakizungumza na kiasi ya waungaji wao mkono 10,000 , viongozi wa upinzani wamesema kuwa Yanukovich anapewa muda hadi katikati ya mwezi Machi mwakani kutia saini makubaliano hayo na Umoja wa Ulaya.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande ameahidi kuwa "mlango wa Umoja huo utaendelea kuwa wazi kwa watu wa Ukraine iwapo watataka."

Mataifa madogo ya Georgia na Moldova wakati huo huo yameanzisha makubaliano ya kisiasa na kibiashara ambayo yatalazimika kutiwa saini rasmi katika miezi ijayo ili kuweza kufanyakazi.

Maandamano nchini UkrainePicha: Reuters

Rais mpya wa Georgia Giorgi Margvelashvili ameyaita makubaliano hayo "siku ya kihistoria kwa Georgia, "siku ya kihistoria kwa Ulaya " lakini akaongeza " tunachukua tahadhari" wakati alipoulizwa iwapo anatarajia kukabiliwa pia na mbinyo kutoka Urusi.

Ameongeza kuwa wanajaribu kutoa ujumbe kwa nchi zote kuwa Georgia yenye ustawi na demokrasia itakuwa kwa manufaa ya majirani zake wote, ikiwa ni pamoja na shirikisho la Urusi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Caro Robi

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW