1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wajadili kuhusu sera ya uhamiaji

28 Juni 2018

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakutana kwa siku mbili mjini Brussels, Ubelgiji katika mkutano wa kilele ambao ajenda yake kuu ni suala la uhamiaji na uwezekano wa kupata sera ya pamoja ya uhamiaji.

EU-Minigipfel
Picha: picture alliance/AP Photo/Y. Herman

Viongozi hao wa nchi 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya mbali na suala hilo tete la uhamiaji pia watajadili biashara kati ya Ulaya na Marekani, uhusiano unaosuasua kati yao na Rais wa Marekani Donald Trump, vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi, bajeti ya muda mrefu ya umoja huo kuanzia mwaka 2021, mageuzi katika kanda inayotumia sarafu ya Euro, mchakato wa kujiondoa rasmi kwa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya ujulikanao kama Brexit miongoni mwa masuala mengine.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Juncker ameonya kuwa viongozi hawapaswi kukurupuka kuchukua maamuzi kuhusu kuanzishwa kwa kile kinachotajwa kuwa maeneo ambayo wahamiaji wa kutoka Afrika watapelekwa bila ya kushauriana kikamilifu na nchi za Afrika Kaskazini.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean Claude JunckerPicha: AFP Photo/J. Thys

Juncker amewataka baadhi ya viongozi kujizuia kuchukua maamuzi kuhusu vituo vya wahamiaji vilivyoko nje ya Umoja wa Ulaya. Mtazamo huo umeungwa mkono na kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye amesema hawawezi kuzungumzia kuzielekeza meli zilizowabeba wahamiaji kwenye nchi nyingine kwa mfano zile za Afrika Kaskazini bali wanahitaji kwanza kufanya mazungumzo na nchi hizo.

Kansela Merkel ambaye anakabiliwa na shinikizo kali nchini Ujerumani kuhusiana na sera yake ya kuwapokea wahamiaji amesema ulinzi wa mipaka ndio jambo linaloliunganisha bara Ulaya na amesema watazungumzia masuala hayo ya ulinzi wa mipaka na kila nyanja ya uhamiaji ikiwemo kuzisaidia nchi zinazowapokea wahamiaji wengi.

Ijapokuwa idadi ya watu wanaokuja barani Ulaya kutafuta hifadhi au maisha bora imeshuka kwa kiasi kikubwa, lakini vyama vinavyopinga wahamiaji vimeimarisha nguvu zao huku vikiwa vinapata ushindi kwenye chaguzi kwa kutumia hoja za hofu juu ya wageni.

Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/Y. Herman

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema Sera ya Umoja wa Ulaya kuhusu wahamiaji imeanza kuleta matokeo mazuri na kwamba nchi wanachama zinahitaji kuendeleza sera hiyo. Bibi Mogherini amesema ni muhimu kuendeleza ushirikiano na marafiki wa Umoja wa Ulaya katika nchi za asili na nchi ambazo zinatumiwa kwa usafirishaji wa watu hasa katika bara la Afrika.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk amesema wameweza kudhibiti mmiminiko wa uhamiaji tangu mwaka 2015 kwa asilimia 96 kwasababu waliamua kushirikiana na nchi zilizo nje ya Umoja wa Ulaya zinazowapokea wahamiaji wengi na kuzuia uhamiaji haramu. Tusk amewahimiza viongozi wanaohudhuria mkutano huo wa kilele kuwa watuame katika suala la kushughulikia mipaka ya nje ya nchi za Umoja wa Ulaya.

Mwandishi:Zainab Aziz/RTRE/DPA

Mhariri: Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW