1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa EU wakabiliana na Orban kuhusu msaada wa Ukraine

1 Februari 2024

Viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya wanajadili msaada wa kifedha kwa Ukraine, wakijaribu kumshawishi waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban kuondoa upinzani dhidi ya euro bilioni 50 kwa taifa hilo linliloko vitani na Urusi.

Ubengiji| Mkutano wa Kilele wa EU-Brussels | Zelenskiy, Orban na Michel
Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban (katikati) ndiye kiongozi pekee anaepinga msada kwa Ukraine.Picha: Virginia Mayo/AP Photo/picture alliance

Idadi kubwa ya viongozi 26 wa mataifa Umoja wa Ulaya wanakubali kwamba usalama wa Ulaya uko hatarini na kwamba suala la muda la umuhimu mkubwa, lakini moja tu ndiyo kikwazo - Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban.

Karibu miaka miwili tangu Urusi iivamie Ukraine, vita hivyo vimekwama, na uchumi wa Ukraine ulioathiriwa vibaya na vita unahitaji kusaidiwa. Lakini malumbano ya ndani ya kisiasa katika Umoja wa Ulaya na nchini Marekani yanainyima Kyiv chanzo muhimu cha ufadhili, ambapo zaidi ya dola bilioni 100 zinazuwiliwa.

Waziri Mkuu Orban, ambaye ni mshirika wa karibu wa Urusi katika Umoja wa Ulaya, alisababisha hasira kutoka kwa wenzake 26 katika kanda hiyo kwa kuzuwia makubaliano ya Desemba ya kuendeleza ufadhili kwa Ukraine.

Akizungumza baada ya kuwasili kwenye mkutano huo, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alisema lengo linapaswa kuwa makubaliano ya pamoja kuhusu kuendeleza mtiririko wa misaada kwa Kyiv.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, amesema lengo la mkutano wa Brussels linapaswa kuwa mufaka wa kuendeleza msaada kwa Kyiv.Picha: Omar Havana/AP/dpa/picture alliance

Ni maani yangu thabiti kwamba hilo lazima liwezekane, ikiwa Ulaya inajifikiria yenyewe kama jumuiya ambayo wote wanasimama pamoja na kusaidiana kufanya maamuzi", alisema Kansela Scholz.

Soma pia: Zelensky ahimiza nchi wanachama wa EU na Marekani kuipa Ukraine misaada zaidi ya kifedha

"Tumeona kwamba nchi wanachama zinajua jinsi uamuzi huo unapaswa kuonekana na kwa hiyo naamini ni wakati wa kuufanya," aliongeza Kansela wa Ujerumani na kuongeza, "na mimi binafsi nitafanya kazi kwa bidii, pamoja na wengine wengi, kuwezesha uamuzi kati ya wanachama 27."

Kazi ngumu kumshinda Orban

Waziri Mkuu wa Ubekgiji Alexander De Croo ameonyesha matumaini, na kusema ana imani katika uwezo wao wa kufikia muafaka na wanachama wote wa Umoja wa Ulaya.

Lakini kumshinda Orban, veterani wa misuguano na Brussels, halitakuwa jambo rahisi na makabiliano ya kisiasa katika mji mkuu wa kisiasa wa Umoja wa Ulaya yanaweza kudumu kwa saa kadhaa.

Orban ambaye ni mfuasi wa siasa za mrengo mkali wa kulia, ametaka kutumia hasira za wakulimwa, ambao malalamiko yao yanahusisha uagizaji wa vyakula vya bei nafuu kutoka Ukraine, uliosababishwa na mzozo, kwa kuchapishwa mtandaoni vidio akiwa anawatembelea Jumatano usiku, ambapo anasikika akizilaumu serikali kwa kutowasikiliza wananchi.

Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban akisalimiana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy nchini Uhispania.Picha: Peter Klaunzer/dpa/KEYSTONE/picture alliance

Orban ameshutumiwa kuushikilia mateka mustakabali wa Ukraine katika jaribio la kuishurutisha Brussels kufungulia mabilioni ya euro za ufadhili wa Umoja wa Ulaya uliozuwiliwa kwa nchi hiyo.

Soma pia: Umoja wa Ulaya washindwa kupata makubaliano kuisidia Ukraine

Baadhi ya viongozi wamekataa pendekezo la Budapest kwamba Orban anaweza kudhinisha msaada huo ikiwa atapata nafasi ya kuuzuwia tena kila mwaka - na badala yake wanampa mjadala wa kila mwaka kuhusu suala hilo.

Iwapo hawawezi kumshawishi Orban kuachana na upinzani wake, viongozi wa Umoja wa Ulaya wameahidi kuungana pamoja kama 26 ili kuendelea kutoa misaada kwa serikali ya Ukraine kuendelea kulipa mishahara na kutoa huduma.

Chanzo: Mashirika